Polisi wapigwa msasa kupambana na ugaidi, uhalifu unaovuka mipaka

New Content Item (1)

Askari polisi kutoka nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, wakipita kwa gwaride mbele ya Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Dk Maduhu Kazi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya utayari, kupambana na vitendo vya ugaidi na uhalifu unaovuka mipaka.

Muktasari:

  • Askari 561 kutoka nchi saba wanachama wa shirikisho la wakuu wa polisi Afrika Mashariki, wamekutana mkoani Kilimanjaro kwa mafunzo ya siku tano, kunolewa namna ya kupambana na vitendo vya kigaidi na uhalifu unaovuka mipaka.

Moshi. Zaidi ya Askari 560 kutoka nchi saba wanachama wa shirikisho la wakuu wa polisi Afrika Mashariki (EAPCCO), wamekutana mkoani Kilimanjaro kwa mafunzo ya siku tano.

Watajifunza namna ya kupambana na vitendo vya kigaidi na uhalifu unaovuka mipaka.

Akizungumza leo Aprili 15, 2024, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya mazoezi ya usalama pamoja, katika Shule ya Polisi Moshi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Maduhu Kazi amesema mafunzo hayo yanatolewa na wataalamu mbalimbali yakilenga kumuwezesha askari polisi kupata mbinu mbalimbali za kupambana na matukio ya uhalifu unaovuka mipaka na ugaidi.

Dk Kazi amesema matukio ya ugaidi na uhalifu unaovuka mipaka hutokea bila kutarajia huku ukihitaji fedha nyingi.

Hivyo, amesema mafunzo hayo yatawasaidia askari hao kupambana na matukio hayo wakati wowote yanapotokea.

Aidha amesema katika mafunzo hayo, pia wataangalia namna nchi hizo zinaweza kuwa na mianya ya kiusalama na ya kimipaka ambayo inaweza kutoa nafasi kwa wahalifu kupenya na kuhatarisha maisha, mali za watu katika ukanda huo.

"Katika mafunzo haya, askari hawa watajifunza pia namna ya kupambana na ugaidi na uhalifu unaovuka mipaka, hapa zipo nchi saba ambazo zimeleta askari 561 na kikubwa watajifunza utayari wa kupambana na matukio hayo katika ukanda huu,” amesema.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Mkuu wa Polisi Tanzania (IGP) Camillius Wambura amesema Tanzania inaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa za kuhakikisha mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka na ugaidi unatokomezwa, ili kuifanya Afrika Mashariki kuwa sehemu salama.

"Mafunzo haya ni kielelezo cha Tanzania kuendelea kuunga mkono utelezaji wa sheria, ulinzi na usalama na kupitia mafunzo haya, polisi wataweza kubadilishana uelewa, mawazo na uzoefu kwa lengo la kuifanya Afrika Mashariki kuendekea kuwa sehemu salama," amesema Wambura.