Polisi wateketeza eka 11 za bangi Iringa

Muktasari:
Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limeteketeza eka 11 za mashamba ya bangi katika kata ya Udekwa wilayani Kilolo, Mkoani Iringa.
Iringa. Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limeteketeza eka 11 za mashamba ya bangi katika kata ya Udekwa wilayani Kilolo, Mkoani Iringa.
Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Allan Bukumbi amesema oparesheni hiyo imefanyika kwa ushirikiano baina yao na Idara ya Maliasili, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Serikali za mitaa.
“Hakuna mtuhumiwa tuliyemkatama kwenye tukio hili, mashamba yote yaliteketezwa kwa kufyekwa na kuchomwa moto,” amesema Bukumbi.
Katika hatua nyingine, Mkazi wa Kijiji cha Mapera Mengi, Wilaya ya Iringa Vijijini Sokoine Ngambusyu anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Iringa baada ya kukamatwa na meno ya tembo.
Bukumbi amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Watu 13 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Iringa baada ya kukutwa na mali mbalimbali za wizi zikiwamo TV, kompyuta mpakati na ving’amuzi.
Katika tukio hilo, Mfanyabiashara wa Manispaa ya Iringa, Franco Monge anadaiwa kumiliki genge la wenzake 12, wakijihusisha na uhalifu.
Kamanda Bukumbi amewataka walioibiwa mali zao kwenda kuzitambua.