Polisi waua watatu wanaodhaniwa ni majambazi

Muktasari:
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limewaua watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi baada ya majibizano ya risasi.
Ngara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limewaua watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi baada ya majibizano ya risasi.
Pia jeshi hilo limekamata silaha aina ya AK 47 isiyokuwa na namba pamoja na magazine moja ikiwa na risasi 12.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, William Mwampaghale amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, amesema watu hao wameuawa wilayani Ngara Novemba 15, 2022.
“Jeshi hili linafanya misako katika maeneo ya mipaka ya Wilaya za Ngara na Biharamlo kufuatia taarifa za kiintelijensia kuwa kuna kikundi cha majambazi kimepanga kufanya uharifu/unyang’anyi kwa kutumia silaha.
“Watu hao walikuwa watano, wawili walifanikiwa kukimbia na watatu ambao majina yao bado hayajafahamika wameuawa”
Amesema katika tukio hilo yalitokea majibizano ya risasi kati ya watu hao watano waliokuwa na silaha na askari polisi ambao waliweka mtego kwa ajili ya kuwakamata.
"Majeruhi hao walifariki wakati wanapelekwa hospitali na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamiyaga Ngara kwa ajili ya kutambuliwa," amesema Mwampaghale.