Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi wawashikilia Wachina wanne kwa utekaji

Raia wa China wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za utekaji wa wafanyabiashara wawili ambao ni Wachina wenzao.


Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Dar es Salaam linawashikilia raia wanne wa China kwa tuhuma za kuwateka wafanyabiashara wenzao na kudai dola milioni 20.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu wanne raia wa China kwa tuhuma za utekaji wa wafanyabiashara wawili ambao ni Wachina wenzao.

Wafanyabiashara hao walitekwa katika majengo pacha ya PSSSF jijini Dar es Salaam wameokolewa na Jeshi la Polisi baada ya operesheni maalumu iliyofanyika Mei 16, 2026.

Akizungumza leo Jumatatu, Mei 25, 2026 kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Mei 14, 2026 saa 7:30 usiku polisi walipokea taarifa za kutekwa kwa Weiyi Chen (64) na Liang Xiolo (44), ambao ni wafanyabiashara na raia wa China.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani leo Jumatatu Mei 25, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema watu hao walivamiwa na kundi la watu saba na kupelekwa kusikojulikana huku watuhumiwa wakianza kutoa vitisho kwa ndugu wa waathirika wakitaka walipwe dola za Marekani milioni 20 (sawa na Sh52.2 bilioni) ili kuwaachia.

"Baada ya uchunguzi kuanza, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuyabaini magari yaliyotumika katika tukio hilo likiwemo Toyota Alphard yenye namba T305 DRA ambazo zilidaiwa kuwa si halali pamoja na Toyota Harrier yenye namba T188 DHT," amesema Muliro.

Amesema operesheni ya uokoaji ilifanikiwa Mei 16, 2026 ambapo waathirika walikutwa katika eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.

Katika uchunguzi huo, amesema Polisi waliwakamata watuhumiwa wanne  akiwemo Fan Zhong (49), Deng Anging  (49), Zhang Jianjun (51) na Deng Qiang wote raia wa China, ambao walikutwa na simu za waathirika  pamoja na vielelezo vingine vinavyohusishwa na tukio hilo.

Raia wa China wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za utekaji wa wafanyabiashara wawili ambao ni Wachina wenzao.

Amesema watuhumiwa wa tukio la utekaji walitumia simu maalumu kupanga na kutekeleza uhalifu huo kabla ya kuzitelekeza baada ya tukio kukamilika.

Kuhusu mwenendo wa uchunguzi huo, Muliro amesema uchunguzi umebaini kuwa simu nne zilitumika kabla na baada ya tukio hilo, lakini baada ya wahusika kutekeleza mpango wao waliziacha na kutumia laini na simu nyingine.

“Walikuwa wanatumia simu nne kabla na baada ya tukio, lakini baada ya kufanya tukio hawakuzitumia tena, wakazitelekeza na kuhamia kwenye simu nyingine,” amesema Muliro.

Amesema pamoja na kwamba kuna taarifa nyingine muhimu za kiupelelezi na ushahidi ambazo haziwezi kuwekwa hadharani kwa sasa, uchunguzi umeonyesha wazi kuwa tukio hilo lilipangwa kwa umakini kabla ya kutekelezwa.

“Huu ulikuwa mpango uliopangwa na kutekelezwa, lakini mhalifu ni mhalifu na uhalifu haulipi,”

Kamanda Muliro amesema watuhumiwa waliokamatwa tayari wamehojiwa na wameeleza mambo mengi yanayosaidia kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo.

Akiweka msisitizo kila mtu aliyeshiriki katika tukio hilo kwa namna yoyote ile atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria huku akibainisha kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kufuata taratibu zote za kisheria katika mchakato wa uchunguzi na mashtaka.

Katika hatua nyingine, Muliro amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kesi nyingine kubwa za uhalifu zilizotokea jijini Dar es Salaam, ikiwemo mauaji ya mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL LI, Bhaozang Ge kilichopo Mabibo Sokoni pamoja na tukio la kutekwa kwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, David  Djumbe.

“Upelelezi wa matukio hayo bado unaendelea na pale tutakapofanikiwa kuwakamata wahusika tutatoa taarifa rasmi kwa umma kama tunavyofanya kwenye matukio mengine,” amesema.

Pia, amewasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu katika jamii.