Polisi wayapa kibano magari ya shule mabovu Shinyanga

Muktasari:

Jeshi la Polisi lataka mabasi hayo yafanyiwe ukaguzi kabla ya kuanza kubeba wanafunzi.

Shinyanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, limepiga marufuku mabasi ya shule yasiyofanyiwa ukaguzi kubeba wanafunzi, huku mawili yakiondolewa namba za usajili baada ya kubainika na ubovu uliokithiri.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Januari 15, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Usalama barabarani wa Mkoa wa Shinyanga, Wenseslaus Gumha baada ya kuyafanyia ukaguzi wa magari ya shule.

Amesema kati ya magari 40 yaliyokaguliwa mawili yamekutwa na ubovu uliokithiri na yameondolewa namba za usajili, huku matano yakikutwa na makosa madogo yakitakiwa kuyarekebishe.

“Ukaguzi huu tulianza shule zilipofungwa Desemba kwa kuyafanyia ukaguzi magari yote ya shule yanayobeba wanafunzi. Tunaendelea na kazi hii kwa kuwa tumebaini hayajafanyiwa ukaguzi,” amesema.

Apolinary Protas  ni mmoja wa madereva wa mabasi ya shule, amesema ukaguzi wa mara kwa mara wa magari, unasaidia kuthibitisha uimara wa mabasi hayo, akisisitiza ni muhimu kazi hiyo iwe endelevu.

Mmiliki wa Shule binafsi, Jacton Koy ameshauri wamiliki wa shule kuzingatia ukaguzi wa magari yanayowabeba wanafunzi, kwa kuwa wanaopanda ni watoto hivyo wanahitaji uangalizi maalum.

Mkazi wa Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, Paul Kiondo amesema baadhi ya madereva hawazingatii sheria za barabarani jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa wanafunzi.