Wamiliki mabasi ya shule yasiyokaguliwa wakamatwa Manyara
Muktasari:
Wamiliki wa shule tatu za Mjini Babati mkoani Manyara, wamekamatwa na polisi baada ya kutotekeleza agizo la kukagua mabasi yanayowabeba wanafunzi pindi shule zikifunguliwa.
Babati. Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Manyara, Georgina Matagi amewaweka mahabusu wamilikiwa wa shule tatu zilizoko mjini Babati kwa kushidwa kupeleka magari ya kubebea wanafunzi ili yafanyiwe ukaguzi na polisi.
Matagi amechukua uamuzi huo Agosti 31 baada ya wamiliki hao kushidwa kitii agizo la kupeleka magari ya shule zao kufanyiwa ukaguzi kabla ya shule kufunguliwa Septemba 5, 2022 ili kubaini magari ambayo ni mabovu.
"Lengo letu ni kuhakikisha magari yanayobeba wanafunzi yanakaguliwa kwani kikubwa ni usalama wa watoto na magari yenyewe pia tumepata funzo kwa ajali iliyotokea Mtwara," amesema Matagi.
Hata hivyo, katika ukaguzi huo amebaini baadhi ya magari hayafai kutumika kutokana na ubovu na akachukua namba za magari hayo ili yaweze kufanyiwa matengenezo ndipo yabebe wanafunzi pindi shule zikifunguliwa.
"Kazi ya ukaguzi wa magari ya shule itaendelea kufanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Manyara na wamiliki wa shule wawe na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa magari ya kubebea wanafunzi mara kwa mara," amesema Matagi.
Pia, amewataka wamiliki wa magari yanayobeba wanafunzi wawe na mikataba na madereva na siyo kuwapa madereva wa mitaani wanaoendesha kwa kutwa.
"Dereva akiwa na mkataba anaweza kumwambia mmiliki kuwa matairi mabovu au gia ina matatizo ili ikafanyiwe matengenezo tofauti na dereva anayeendesha kwa kutwa," amesema Matagi.
Mmoja kati ya madereva wa magari yanayobeba wanafunzi Simon John amepongeza hatua hiyo ya ukaguzi wa magari kwani itaepusha ajali zisizo za lazima.
"Pia Afande RTO ametoa namba zake kwa madereva ili tukinyimwa haki zetu tumjulishe aweze kutusaidia pindi wamiliki wa magari hayo wakitunyanyasa," amesema.