Vijana waelekezwa kutumia mitandao kujikwamua kiuchumi
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akifungua kongamano la vijana katika wilaya hiyo. Picha na Samwel Mwanga
Muktasari:
- Matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kubadili maisha ya vijana wengi ikiwa wataamua kuitumia kujifunza ujuzi, kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kuanzisha biashara kupitia majukwaa ya kidijitali.
Maswa. Vijana nchini wamehimizwa kuacha kutumia vibaya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali, badala yake waielekeze katika kutafuta mafunzo, ajira na fursa za biashara zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa, Julai 24, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano, wakati akifungua Kongamano la Vijana la Wilaya ya Maswa lililofanyika wilayani humo chini ya kaulimbiu, "Vijana Tuyajenge, Tanzania Ni Yetu Sote."
Dk Naano amesema matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kubadilisha maisha ya vijana wengi iwapo wataitumia kujifunza ujuzi, kutangaza bidhaa na huduma pamoja na kuanzisha biashara kupitia majukwaa ya kidijitali.
"Mitandao ya kijamii isiwe sehemu ya kupoteza muda au kusambaza taarifa zisizo na manufaa. Itumieni kujifunza, kutafuta masoko ya bidhaa zenu na kuanzisha biashara zitakazowaongezea kipato," amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, huku akiwataka kutumia ipasavyo fursa mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kujiletea maendeleo binafsi na ya taifa.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Maswa, Hollo Ngeme amesema kongamano hilo limeandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha vijana na kuwapa nafasi ya kujadili masuala yanayogusa maisha yao pamoja na maendeleo ya taifa.
Amesema mada zilizowasilishwa zilihusu utawala bora, elimu ya uraia, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, fursa za kiuchumi, vita dhidi ya rushwa, matumizi ya dawa za kulevya na falsafa ya Mwenge wa Uhuru.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema zaidi ya vijana 300 kutoka kata zote 36 za wilaya hiyo walishiriki kongamano hilo.
Amesema lengo la kongamano ni kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika maamuzi ya maendeleo, kuongeza uelewa wa haki na wajibu wao, pamoja na kuwahamasisha kutumia maarifa wanayopata kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.
Baadhi ya vijana walioshiriki kongamano hilo walisema mafunzo waliyoyapata yamewabadilisha mtazamo kuhusu matumizi ya teknolojia na fursa zilizopo kupitia mitandao ya kijamii.
Neema Joseph kutoka Kata ya Nyalikungu amesema amegundua kuwa simu ya mkononi inaweza kuwa nyenzo ya kujiongezea kipato badala ya kutumika kwa burudani pekee.
"Nimegundua kuwa simu niliyokuwa nikiitumia kwa burudani pekee inaweza kuwa chanzo cha kipato. Nitaanza kuitumia kutafuta mafunzo na kutangaza biashara ndogo ninayofanya," amesema.
Kwa upande wake, Juma Jongela kutoka Kata ya Sola amesema kongamano hilo limewapa vijana hamasa ya kujitegemea badala ya kusubiri ajira rasmi.
"Tumeelezwa namna ya kutumia teknolojia kupata wateja na kuanzisha biashara. Haya ni maarifa muhimu yatakayotusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira," amesema.
Naye Asha Mohamed kutoka Kata ya Senani amesema elimu kuhusu rushwa, matumizi ya dawa za kulevya na ukatili wa kijinsia imewapa vijana uelewa mpana kuhusu wajibu wao katika jamii.
"Sisi vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa. Tukitumia mitandao ya kijamii kwa tija na kuzingatia maadili, tunaweza kujenga uchumi wetu na kuchangia maendeleo ya Wilaya ya Maswa na Tanzania kwa ujumla," amesema.