Polisi yatakiwa kusajili mali kielektroniki

Katibu Mkuu wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio akizungumza wakati akifungua kikao kazi kinachofanyika katika Shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio amelitaka jeshi la polisi nchini kusajili mali zake zote katika mfumo wa kielektroniki wa utunzaji wa kumbukumbu za mali.

Moshi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio amelitaka jeshi la polisi nchini kusajili mali zake zote katika mfumo wa kielektroniki wa utunzaji wa kumbukumbu za mali.

Kadio ametoa agizo hilo leo Jumatano Novemba 24, 2021 wakati akifungua kikao kazi cha wakuu wa usalama barabarani, maafisa wanadhimu na wahasibu wa mikoa, vikosi na vyuo vya polisi kinachofanyika katika ukumbi wa Shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema jeshi hilo lina mali nyingi ambazo hazijaingizwa kwenye mfumo wa kielektroniki wa utunzaji wa kumbukumbu na kuagiza ameligiza jeshi hilo kuhakikisha mali zote ziwe tayari zimesajiliwa kwenye mfumo huo ifikapo Juni 2022.

"Serikali imeanzisha mfumo mpya wa kielektroniki wa utunzaji wa kumbukumbu za mali za Serikali, Jeshi la Polisi lina mali nyingi ambazo bado hazijaingizwa kwenye daftari hili kutokana na sababu mbalimbali, kuna usemi unasema mali bila daftari hupotea bila habari"

Ameongeza kuwa "Niagize jambo hili halina budi kulikamilisha na tusizidi Juni 2022, kaeni mjipange muone mahitaji na changamoto mzitafutie ufumbuzi mapema na muwasiliane na wenzetu wa hazina ili kazi hii ifanyike kama tulivyoelekezwa na Serikali"

Akizungumzia changamoto ya madeni ya watumishi, wazabuni na wale waliotoa huduma mbalimbali kwa jeshi hilo, katibu mkuu amesema serikali imedhamiria kulipa madeni yote yaliyohakikiwa.

"Kwa kipindi kirefu kumekuwa na madeni ya watumishi, wazabuni na watoa huduma mbalimbali ambao wanalidai jeshi la polisi baada ya kutoa huduma, Serikali imedhamiria kulipa madeni yote ambayo yamehakikiwa na yale ambayo hayajahakikiwa, hazina imetuma wakaguzi, ambao wapo wanaendelea na kazi"

"Tuhakikishe madeni yote yanahakikiwa na kunakuwepo na nyaraka zote kabla ya kuanza kusema Serikali haijalipa na nitawashangaa mkoa ambao utaleta madeni halafu hawana nyaraka".

Kamishna wa fedha na lojistiki, Hamad Hamisi Hamad amesema Jeshi hilo linakabiliwa changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa watumishi, manung'uniko ya kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu, uchakavu wa vifaa vya kukusanyia maduhuli pamoja na madeni ya muda mrefu ya watumishi, wazabuni na watoa huduma.