Polisi yawakamata watoto wa mitaani 22 Iringa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Allan Bukumbi akizungumza na wanahabari Mkoani Iringa kuhusu tukio la watoto kukamatwa wakitumiwa kufanya uhalifu.
Muktasari:
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewakamata watoto wa mitaani 22 kwa tuhuma za kutumiwa kufanya uhalifu wa matukio mbalimbali.
Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewakamata watoto wa mitaani 22 kwa tuhuma za kutumiwa kufanya uhalifu wa matukio mbalimbali.
Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Desemba 7, 2021 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema kuwa siku za hivi karibuni kulijitokeza uhalifu ambapo watoto wadogo wa mitaani wamekuwa wakitumiwa na wahalifu katika matukio mbalimbali ya uhalifu.
“Kufuatia kukamatwa kwa watoto hao katika matukio mbalimbali ya uhalifu Jeshi la Polisi lilifanya upelelezi na kubaini kuwa watoto hawa wanatumwa na watu wazima kufanya uhalifu na watoto wenyewe kufanya uhalifu kutokana na baadhi ya vituo vya malezi kufungwa hivyo watoto hao kukosa huduma” amesema Bukumbi
Bukumbi amesema kuwa taratibu za kuwaunganisha watoto hao na familia zao zinaendelea huku watoto 6 tayari wamekabidhiwa kwa wazazi wao na baada ya zoezi hilo kukamilika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wazazi au walezi ambao watatelekeza watoto wao.
Wiki iliyopita Mkuu wa dawati la jinsia na watoto, Elizabeth Swali aliitaka jamii kushirikiana kabla Jeshi la Polisi halijaanza kufanya msako kwa kuwalea watoto wao vizuri na inapotokea vitendo vya ukatili au changamoto yeyote watoe taarifa ili waweze kuchukua hatua kwa pamoja.
“Tunafanya jitihada mbalimbali za kupunguza na kukomesha kabisa vitendo vya ukatili kwa Mkoa wa Iringa kwa kutoa elimu kwa jamii ili waweze kuondokana na sula la ukatili kwa kuwa baadhi ya matendo ya ukatili yapo kama mazoea, mila na desturi na ulevi”amesema Swai
Swai amesema kuwa watoto wengi wakiwakamata wanawarudisha katika familia zao na wengine kuwapeleka katika mashirika mbalimbali ambayo yanaweza kutoa misaada kwa kuwalea watoto hao.
“Sababu kubwa za kuwepo kwa watoto wa mitaani linachangiwa na ukatili wengi wanafanyiwa ukatili wengine ni yatima wanakaa na wazazi wa kambo hawana uangalizi mzuri kutoka katika familia zao, tatizo hili la ukatili kwa mkoa wa Iringa ni kubwa kwa sababu hujitokeza mara kwa mara”
Mmoja wa watoto hao “Tunaiomba Serikali itusaidie kuturudisha majumbani kwa wazazi na walezi wetu ili tuendelee kupata malezi bora ya wazazi chini ya uangalizi wa polisi”
Ameongeza “Mimi niliamua kutoroka nyumbani kwetu Makambako baada ya mama yangu kufariki na baba kuoa mke mwingine na mama yule alianza kunitesa nikawa siendi shule chakula sipewi nikaona nitoroke nije Iringa kutafuta maisha”