Polisi yawapa mbinu kina baba wanaopigwa, kunyimwa unyumba

Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi wa pili kutoka kushoto akiwa katika picha ya pamoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Mtwivila ya viziwi iliyopo mjini Iringa.

Muktasari:

  • Kamanda huyo amesema kina baba wanaofanyiwa ukatili lakini hawaendi dawati, mnakufa na tai shingoni mnaona aibu mwishoni mnaamua kujinyonga msikae kimya njooeni dawati" amesema Kamanda Lydia

Iringa. Kamanda Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Mkoani Iringa, Lydia Sospeter amesema wapo baadhi ya wanaume wanapitia madhira ya ukatili katika ndoa kama vipigo na kunyimwa unyumba na wenza wao lakini wanaona aibu kufika kituo cha polisi kuripoti ukatili huo.

Kamanda huyo amesema kina baba wanaofanyiwa ukatili lakini hawaendi dawati, mnakufa na tai shingoni mnaona aibu mwishoni mnaamua kujinyonga msikae kimya njooeni dawati" amesema Kamanda Lydia

Hayo yamesemwa na ofisa huyo wa jeshi wakati wakiongozwa na Kamanda wa Polisi mkoani hapo, Allan Bukumbi kufanya usafi katika soko Kuu la manispaa ikiwa ni hatua ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Zoezi hilo limefanyika leo JanuarI 23,2023 pamoja na utoaji wa elimu juu ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ambayo yanazidi kushamiri Mkoani hapa.

Akizungumza na wafanyabiashara wa soko kuu Iringa Baada ya kutamatisha zoezi la kufanya usafi katika soko hilo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa Allan Bukumbi amesema wamefanya zoezi hilo kuelekea Siku ya Polisi Kulinda Afya ya Wananchi.

Sambamba na zoezi la usafi pia wafanyakazi hao wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa wametoa msaada katika Shule ya Msingi Viziwi iliyopo mkoani Iringa na kukata keki na kucheza mpira pamoja na watoto hao ambao wanaulemavu wa kusikia na kuongea.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi, Mkoani Iringa Elizabeth Swai  amewaasa wanafunzi qa shuke ya Msingi Viziwi iliyopo Mtwivila Mjini Iringa kutoa taarifa kwa polisi endapo wataona wapo katika mazingira hatari yenye viashiria vya ukatili wa kijinsia.

Kamanda Swai amesema kuwa kwa sasa ukatili umekithiri kwa watoto na wanafanyiwa ndani ya familia zao jambo ambalo linasababisha ndoa nyingi kuvunjiaka.

Swai amesema kuwa kumkatili kijinsia mtoto mdogo ni kumuharibi kisaikolojia na kusababisha watoto wengi kuharibikiwa kutokana na vitendo hivyo.

"Nawashauri watoto wanaofanyiwa ukatili wasiogope kutoa taarifa dawati ili wapewe msaada wa kisheria na kisaikolojia kwa sababu unaweza kuona ni kiziwi hasikii wala haongei, ukamfanyia ukatili kwa sababu hawezi kujieleza, lakini niwahakikishie Jeshi la Polisi limejipanga na tuna kitengo maalumu kwa ajili ya kutetea haki ya kila mmoja," amesema.