Popo wageuka kero Kigamboni, Serikali yaeleza changamoto kila inapowaondoa

Muktasari:

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ameiomba Serikali kupeleka haraka watalaam katika kata ya Kivukoni jijini Dar es Salaam ili wakawaondoe popo waliogeuka kero.



Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ameiomba Serikali kupeleka haraka watalaam katika kata ya Kivukoni jijini Dar es Salaam ili wakawaondoe popo waliogeuka kero.

Zungu amesema popo hao wamekuwa tatizo katika maeneo hayo, wanasumbua wananchi na  wamezaliana sana.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema wakati wowote kabla ya kumalizika kwa vikao vya Bunge, Serikali itapeleka wataalamu kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kwenda kuwaondoa popo hao.

Hata hivyo, Masanja amesema si mara ya kwanza kuwaondoa popo katika kata hiyo na maeneo yanayozunguka Ikulu lakini kumekuwa na changamoto kila wanapopuliziwa dawa huwa wanaruka.

 “Ni kweli popo wamekuwa kero kubwa katika maeneo hayo ikiwemo eneo la kuzunguka Ikulu, wanafanya uchafuzi kwenye maeneo hayo lakini hii si mara ya kwanza kuwafukuza ila huwa wanaruka wanapopuliziwa dawa, nikuhakikishie kuwa kabla ya mkutano huu kumalizika tutafanya kazi hiyo,” amesema Masanja.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Nanyumbu (CCM), Ally Mhata ameuliza ni wananchi wangapi wa Nanyumbu wamefidiwa kutokana na uharibifu uliofanywa na tembo katika mashamba yao.

Wizara hiyo imesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2022/23 ilipokea jumla ya maombi nane kutoka kwa wananchi wa vijiji vya Mchenjeuka, Lukula, Masuguru, Marumba na Mpombe ambao waliathiriwa na wanyama pori.

Amesema Jumla ya Sh5.1 milioni zililipwa kwa wananchi saba lakini mwezi Machi mwaka huu Serikali imepokea tena maombi ya watu 12 katika jimbo hilo ambao kwa sasa wanaendelea kuyafanyia kazi.

Kwa upande mwingine Naibu Waziri amesema kwa sasa Serikali inafanya mkakati wa kupeleka bungeni kanuni za malipo ya kifuta machozi kwa wanaoathiriwa na wanyama.