Profesa Janabi aonya kuhusu sukari, akikabidhi msaada waathirika wa mafuriko Rufiji

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge akizungumza na mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la THPS, Profesa Mohamed Janabi  baada ya kukabidhi msaada wa vyakula na vifaa vya shule kutoka shirika hilo kwa waathirika wa mafuriko wilayani Rufiji na Kibiti. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Arejea maisha ya mwanadamu miaka 300 kabla ya ugunduzi wa sukari.

Kibaha. Miaka 300 iliyopita duniani hakukuwa na sukari, hali inayoelezwa iliwaepusha binadamu kupata magonjwa yanayotokana na matumizi ya bidhaa hiyo.

 Kutokana na hilo, imeelezwa wakati umefika sasa wa kuitumia sukari kwa makini kulinda afya.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya THPS (Tanzania Health Promotion Support), Profesa Mohamed Janabi amesema hayo alipokabidhi msaada wa vyakula, mavazi na vifaa vya shule kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge.

Msaada huo wenye thamani ya Sh18.8 milioni ni kwa ajili ya waathirika wa mafuriko katika wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani.

"Shirika limeleta unga wa sembe, maharage, mafuta ya kupikia, sare za shule, madaftari na sukari, lakini hili la sukari sikuhusishwa.

"Hii ni bonasi kwa wote hapa tunaposema sukari si ile ya kijiko pekee, bali hata matunda yake, tamutamu tupunguze kutumia ili kulinda afya zetu," amesema.

Amesema historia inaonyesha miaka 300 duniani hakukuwa na sukari na watu waliishi na afya njema, hivyo kama jamii itazingatia kupunguza matumizi hayo itawaepusha na madhara yatokanayo na bidhaa hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dk Redempta Mbatia amesema pamoja na mambo mengine, shirika hilo kwa sasa linalenga kushughulikia changamoto za afya ya umma ikiwa ni pamoja na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, kifua kikuu na ukatili dhidi ya watoto.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kunenge amesema ingawa mafuriko hayo yameathiri mali na makazi ya wananchi hao, jambo la kushukuru ni kuwa mpaka sasa wanaendelea vizuri.

Amesema wanakabiliwa na changamoto ya kukosa mahitaji muhimu ikiwemo chakula na makazi.

“Nashukuru Serikali imeonyesha dira juu ya kutoa misaada, wadau wengi wameendelea kuiga mfano huo. Naomba na taasisi zingine ziige mfano huo," amesema.

Mkazi wa Kibiti, Bakari Mgage amesema jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali kwa kutoa misaada ya vyakula na mavazi imewapunguzia makali.

Amesema anaamini hata msaada uliotolewa na THPS utawafikia walengwa kama inavyostahili na utaongeza faraja kwa waathirika.