Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Janabi azitaka nchi za Afrika kuwekeza kwa wataalamu wa afya

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ukanda wa Afrika Mohamed Janabi akizungumza katika mkutano wa Mkapa Legacy Summit' Dar es Salaam

Muktasari:

  • Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF) imetangaza mkakati wa kupanua shughuli zake barani Afrika na kuwekeza katika kuandaa kizazi kipya cha viongozi wa afya, ikisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha urithi wa hayati Rais Benjamin Mkapa unaendelea kutoa mchango kwa vizazi vijavyo.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, amezitaka nchi za Afrika kuongeza uwekezaji katika rasilimali watu kwenye sekta ya afya, akisema mustakabali wa bara hilo unategemea kuwawezesha vijana kwa kuwapa ujuzi, fursa za ajira na nafasi za uongozi.

Profesa Janabi amesema hayo leo Alhamisi, Julai 16, 2026, katika mkutano wa nne wa urithi wa hayati Rais Benjamin Mkapa, pamoja na maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF), yaliyofanyika Dar es Salaam.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyeambatana na mlezi wa taasisi hiyo na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Ellen Mkondya-Senkoro akizungumza na wageni waliohudhuria mkutano unaozungumzia urithi Benjamin Mkapa 'Mkapa Legacy Summit'

Profesa Janabi amesema urithi wa hayati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, unaonesha kuwa maendeleo endelevu hupatikana kupitia uwekezaji kwa watu na ujenzi wa taasisi imara zinazohudumia wananchi.

Amesema kati ya mwaka 2022 na 2024, Afrika ilizalisha wataalamu wa afya 500,000, lakini mafanikio hayo yako hatarini kupotea iwapo serikali hazitaweka mazingira yatakayowawezesha wataalamu hao kupata ajira na kuendelea kufanya kazi katika nchi zao.

"Ni lazima tuwekeze katika kuwabakiza wataalamu wetu wa afya. Bila fursa za ajira, mazingira bora ya kazi na maendeleo ya taaluma, tutazidi kupoteza nguvu kazi muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya," amesema.

Profesa Janabi amesema WHO itaendelea kushirikiana na nchi wanachama kutekeleza Ajenda ya Rasilimali Watu Sekta ya Afya Afrika ya mwaka 2026–2035, inayolenga kuongeza idadi ya watumishi wa afya, kuwajengea uwezo, kuwaajiri na kuwabakiza kazini ili kufanikisha huduma za afya kwa wote.

Katika mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Ellen Mkonya-Senkoro, ametangaza mkakati wa kupanua shughuli za taasisi hiyo barani Afrika na kuwekeza katika kuandaa kizazi kipya cha viongozi wa afya.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha urithi wa hayati Mkapa unaendelea kutoa mchango kwa vizazi vijavyo.

Dk Mkonya-Senkoro amesema baada ya miaka 20 ya utekelezaji wa miradi nchini Tanzania, taasisi hiyo imejifunza kuwa changamoto nyingi za afya zinazoikabili Afrika zinaweza kutatuliwa kwa kutumia uzoefu uliopatikana nchini.

"Tunaamini mipaka ya Tanzania si mwisho wa safari yetu. Tunataka kuchukua uzoefu tulioupata hapa na kuushirikisha mataifa mengine ya Afrika ili kujenga taasisi inayoongoza katika maendeleo ya afya barani," amesema.

Amesema taasisi hiyo pia imeanzisha Mpango wa Uongozi wa Afya (Mkapa Health Leadership Programme), utakaowajengea uwezo viongozi vijana wa Afrika kushiriki katika utungaji wa sera za afya duniani.

Kwa mujibu wake, kwa muda mrefu Afrika imekuwa ikifuata uamuzi unaofanywa na wengine kuhusu sekta ya afya badala ya kushiriki kikamilifu katika kuyaunda.

"Tunataka kuona Waafrika wanakuwa watunga sera, si wapokeaji wa sera pekee. Huo ndio mwelekeo wetu mpya," amesema.

Aidha, amesema taasisi itaendelea kuwekeza katika ubunifu wa kidijitali unaoongozwa na vijana ili kuimarisha mifumo ya afya ya umma. Amebainisha kuwa tayari asilimia 80 ya maazimio yaliyotolewa na vijana katika mkutano wa tatu wa rasilimali watu sekta ya afya mwaka 2024 yameanza kutekelezwa na Serikali.

Akizungumzia mafanikio ya taasisi hiyo, Dk Mkonya-Senkoro amesema kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, BMF imewafikia zaidi ya watu milioni 33 nchini na kukusanya zaidi ya Sh450 bilioni kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya.

Amesema pia taasisi hiyo imewezesha zaidi ya wahitimu 8,000 wa programu ya Mkapa Fellows, pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii zaidi ya 11,000, kuhudumu katika maeneo yenye upungufu wa wataalamu wa afya. Aidha, imejenga au kukarabati vituo vya afya 520 na nyumba 480 za watumishi wa afya vijijini.

Wageni mbalimbali waliohudhuria mkutano wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa 'Mkapa Legacy Summit' uliofanyika Dar es Salaam

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema alipoteuliwa kuongoza mkoa huo alijiuliza aina ya watu ambao angefanya nao kazi katika uongozi wake.

Akimnukuu hayati Rais Benjamin Mkapa, Chalamila amesema uwekezaji katika rasilimali watu ndiyo msingi wa maendeleo endelevu.

"Hayati Benjamin Mkapa aliwahi kusema kuwa kama nchi haijawekeza katika mtaji wa watu, ni vigumu kuwa na maendeleo endelevu kama taifa," amesema.

Ameongeza kuwa kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam wenye makundi mbalimbali ya watu si kazi rahisi na wakati mwingine amekuwa akilaumiwa kwa mtindo wake wa uongozi kutokana na changamoto zinazotokana na wingi na tofauti za wananchi.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni muhimu taifa kuendelea kuwekeza katika watu ili idadi kubwa ya wananchi iwe rasilimali yenye tija kwa maendeleo ya nchi.