Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afrika yatakiwa kubadili mfumo wa kuandaa wataalamu wa afya

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe

Muktasari:

  • Wataalamu wa Afya wamezitaka nchi za Afrika kufanya mageuzi ya rasilimali watu sekta ya afya kwa kuwekeza kwenye ajira, teknolojia na mipango ya muda mrefu ili kufikia huduma za afya kwa wote ifikapo 2040.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamezitaka nchi za Afrika kufanya mageuzi ya mfumo wa kuandaa, kuajiri na kusimamia rasilimali watu sekta ya afya ili kufikia lengo la huduma za afya kwa wote ifikapo 2040.

Wamesema badala ya kuendelea kuwekeza kuongeza idadi ya madaktari na wauguzi pekee, nchi zinapaswa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa teknolojia za kidijitali na mgawanyo sawa wa rasilimali watu kati ya mijini na vijijini yenye uwezo wa kukabiliana na majanga na kujibu mahitaji mapya ya  sekta hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 15,2026 na  Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe wakati  akizungumza kwenye mkutano wa rasilimali watu sekta ya afya ulioandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa.

Dk Kapologwe amesema Afrika imeongeza idadi ya wataalamu wa afya hadi kufikia  milioni sita, lakini bado inakabiliwa na upungufu wa asilimia 46 ya nguvu kazi inayohitajika kuhudumia idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi.

“Ni jambo la kushangaza kuona tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa afya wakati huohuo maelfu ya wahitimu wanabaki bila ajira, hili inaonyesha changamoto si uzalishaji wa wataalamu pekee, bali uwezo wa nchi kuwatumia na kuwahifadhi,” amesema.

Wataalamu wa Afya wakiwa kwenye mjadala unaohusu rasilimali watu ulioandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa.

Amesisitiza msingi wa huduma bora za afya unabaki kuwa watu, akieleza maendeleo ya teknolojia hayawezi kuchukua nafasi ya utu na huruma wakati wa utoaji wa huduma.

“Watu ndiyo wanaowaponya watu, dawa hazijitibu zenyewe, sera haziwezi kumfariji mgonjwa na teknolojia haiwezi kuchukua nafasi ya huruma ya mtoa huduma,” amesema.

Dk Kapologwe ameonya ifikapo 2050 idadi ya watu barani Afrika inatarajiwa  kuongezeka maradufu, hali itakayoongeza mahitaji ya huduma za afya ya mama na mtoto, matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza, huduma kwa wazee na uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya.

Kutokana na hali hiyo, amesema serikali za Afrika haziwezi kuendelea kupanga rasilimali watu kwa kuzingatia mahitaji ya sasa pekee, bali zinapaswa kuwekeza katika mipango ya muda mrefu itakayojenga mfumo wa afya unaokidhi mahitaji ya vizazi vijavyo.

Amesema nguvu kazi ya afya ya mwaka 2040 inapaswa kuwa tofauti na ya sasa kwa maarifa, ujuzi na uwezo wa kukabiliana na mazingira mapya ya utoaji huduma.

Kwa mujibu wake, mfumo mpya wa rasilimali watu kwa afya unapaswa kujengwa katika nguzo saba muhimu ambazo ni kuwa na idadi ya kutosha ya wataalamu, usambazaji wenye uwiano kati ya mijini na vijijini.

Pia matumizi ya teknolojia za kidijitali, ushirikiano wa taaluma mbalimbali, uwezo wa kukabiliana na majanga ya afya, ushindani katika soko la kimataifa na kujitolea kuhudumia jamii.

Aidha, amesema mtaalamu wa afya wa baadaye atalazimika kufanya kazi sambamba na teknolojia za akili unde badala ya kuziona kama tishio.

“Daktari wa baadaye hatashindana na akili unde, atafanya kazi sambamba nayo. Mtaalamu wa afya wa kesho anatakiwa awe na uwezo wa kutumia stethoscope pamoja na dashibodi za kidijitali kwa wakati mmoja,” amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa rasilimali watu sekta ya afya, Rahel Sheiza, amesema makadirio yanaonyesha Afrika itakuwa na upungufu wa wataalamu wa afya wapatao milioni 6.1 ifikapo mwaka 2040, huku juhudi zinazofanyika sasa zikitarajiwa kukidhi takribani asilimia 49 tu ya mahitaji.

Amesema hali hiyo inaonyesha kuongeza idadi ya wahitimu pekee hakutatosha bila kuwepo sera zinazowezesha kuajiri na kuwahifadhi wataalamu hao.

“Bado tunaona wataalamu wengi waliopata mafunzo hawana ajira wakati vituo vya afya vina uhaba mkubwa wa watumishi. Serikali zinapaswa kuwekeza zaidi katika kuunda nafasi za kazi zenye hadhi na mazingira yanayowavutia wataalamu kubaki nchini,” amesema.

Sheiza amependekeza serikali kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya sekta ya afya na kutumia mifumo bunifu ya ufadhili ikiwemo ushiriki wa sekta binafsi, ununuzi wa kimkakati wa huduma na mifumo ya malipo inayozingatia utendaji ili kuongeza motisha kwa watumishi wa afya.

Ameongeza kuwa Afrika haiwezi kufikia malengo ya ajenda 2063 bila kujenga nguvu kazi ya afya inayotumia teknolojia na ubunifu katika utoaji wa huduma.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Siana Nkya, amesema Tanzania imeanza kuwekeza katika sayansi ya tiba zinazolenga mahitaji ya mgonjwa mmoja mmoja, hatua itakayoiwezesha kuwa sehemu ya mifumo ya kisasa ya afya.

“DNA ya binadamu ina taarifa muhimu kuhusu namna mwili unavyofanya kazi, jinsi unavyoathiriwa na magonjwa na namna unavyoitikia dawa. Uelewa wa taarifa hizi utasaidia kutoa huduma za afya zilizo sahihi zaidi kwa kila mgonjwa,"amesema.