Prime
Wataalamu wapendekeza sheria kudhibiti elimu ya afya mitandaoni
Muktasari:
- Afya ya uzazi ndiyo eneo linaloathirika zaidi, kutokana na kuwa miongoni mwa mada zinazovutia vijana wengi wanaotumia mitandao ya kijamii.
Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamependekeza Serikali kutunga sheria itakayodhibiti utoaji wa elimu ya afya kupitia mitandao ya kijamii ili kupunguza ongezeko la taarifa potofu zinazohatarisha maisha ya wananchi.
Pendekezo hilo limekuja siku chache kufuatia wito wa Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi kuwataka wataalamu wa afya kutumia zaidi majukwaa ya kidijitali kutoa elimu kwa umma, badala ya kuwaachia watu wasiokuwa na taaluma kujaza mitandaoni ushauri usiozingatia misingi ya kisayansi.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 8, 2026 Daktari bingwa wa upasuaji katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Mugisha Nkoronko amesema pamoja na kuhamasisha wataalamu kujitokeza kutoa elimu, bado kuna haja ya kuwa na sheria itakayoweka utaratibu wa nani anapaswa kutoa taarifa za afya kwa umma.
"Nadhani umefika wakati wa kuwa na sheria ya afya itakayodhibiti utoaji wa elimu ya afya mitandaoni. Sheria hiyo iweke wazi nani anaruhusiwa kutoa elimu ya afya, kiwango cha taaluma anachopaswa kuwa nacho na namna ya kuthibitisha sifa zake," amesema Dk Nkoronko aliyekuwa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).
Amesema kukosekana kwa mfumo wa udhibiti, kumechangia watu wengi wasiokuwa na taaluma, kujitangaza kama wataalamu wa afya na kutoa ushauri unaowafanya baadhi ya wananchi kutumia dawa na tiba ambazo hazijathibitishwa.
Suala sawa na hilo liliwahi kukemewa na kutolewa maagizo Aprili 7 mwaka huu na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akitilia mkazo zaidi msako wa wauza vipodozi na dawa mitandaoni.
“Suala hili liliundiwa kamati kutoka Wizara ya Afya, Wizara ya Viwanda na Biashara na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, bado taarifa haijatoka hivi karibuni itakuja na majibu,” amesema Kaimu Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini – Wizara ya Afya, Said Makora.
Kwa mujibu wa Dk Nkoronko, afya ya uzazi ndiyo eneo linaloathirika zaidi kutokana na kuwa miongoni mwa mada zinazovutia vijana wengi wanaotumia mitandao ya kijamii.
"Kwa sasa, Tanzania ina idadi kubwa ya vijana. Hivyo maudhui yanayohusu afya ya uzazi, ugumba na nguvu za kiume yanapata wasikilizaji wengi. Lakini hali tunayoshuhudia mitandaoni haiendani na ukubwa wa matatizo tunayoyaona hospitalini," amesema.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia dawa zenye dozi kubwa au ambazo hazijafanyiwa uthibitisho wa kisayansi, baada ya kushauriwa na watu wasiokuwa wataalamu.
"Wengine wameharibu viungo vyao kwa kutumia dawa hizo. Badala ya kupata tiba wamejikuta wakipata matatizo makubwa zaidi. Ndiyo maana ni muhimu wataalamu wajitokeze kutoa elimu na Serikali ichukue hatua dhidi ya wanaopotosha umma," amesema.
Dk Nkoronko amesema nchi mbalimbali zimeweka mifumo ya kuhakikisha maudhui ya afya yanayotolewa kupitia majukwaa ya kidijitali yanatokana na watu wenye sifa na vyanzo vinavyoaminika, akisisitiza Tanzania inaweza kufanya hivyo kupitia sheria.
Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Misheni ya Ifakara, Elias Kweyamba amesema elimu ya afya inapaswa kutolewa na wataalamu wa eneo husika, kwa sababu kila taaluma ina utaalamu wake.
"Ni vyema elimu ya afya ya uzazi ikatolewa na wataalamu wa afya ya uzazi. Taarifa unazoziona mtandaoni si zote ni sahihi na mara nyingi usahihi wake hutegemea chanzo chake," amesema.
Amesema taarifa nyingi zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii huongeza hofu na wakati mwingine hupotosha ukweli kuhusu masuala mbalimbali ya afya ya uzazi.
"Kuna upotoshaji kwenye karibu maeneo yote ya afya ya uzazi, lakini unaonekana zaidi kwenye masuala ya ugumba na nguvu za kiume. Haya ndiyo maeneo yanayowafanya watu wengi kukimbilia tiba zisizo sahihi," amesema.
Dk Kweyamba amesema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa wananchi kuwasikiliza wataalamu waliobobea katika maeneo husika, badala ya kufuata ushauri wa watu maarufu mitandaoni wasio na taaluma ya afya.
‘Taarifa potovu’
Naye mtaalamu wa elimu ya afya ya uzazi mashuleni, Mgeni Kisesa amesema pamoja na mitandao ya kijamii kuwa njia muhimu ya kusambaza taarifa, imekuwa pia chanzo cha kuenea kwa taarifa potofu kuhusu afya ya uzazi.
Amesema taarifa hizo zinaweza kuwafanya wananchi kufanya maamuzi yasiyo sahihi kuhusu uzazi wa mpango, ujauzito na huduma nyingine muhimu za afya ya uzazi.
"Ni muhimu wananchi wakapata taarifa kutoka kwa wataalamu wa afya na taasisi zinazotambulika. Pia kunahitajika kuimarisha kampeni za elimu kupitia majukwaa ya kidijitali na kuwajengea wananchi uwezo wa kutambua taarifa sahihi kabla ya kuzitumia au kuzisambaza," amesema.
Amesema ushirikiano kati ya wataalamu wa afya, vyombo vya habari na wadau wa maendeleo utasaidia kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi zitakazoiwezesha kufanya maamuzi bora kuhusu afya.
Kauli za wataalamu hao zinaibua mjadala kuhusu namna ya kulinda uhuru wa kutoa maoni mtandaoni, huku ikihakikisha elimu ya afya inayowafikia wananchi inatolewa kwa kuzingatia taaluma, ushahidi wa kisayansi na maadili ya kada ya afya.
Julai 4, 2026 akizungumza na walimu, viongozi na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Mucohas), Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi aliagiza wataalamu wa afya nchini kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu sahihi kwa wananchi na kutowaachia watu wasio na utaalamu, kuendelea kusambaza taarifa zinazoweza kupotosha kuhusu masuala ya afya.
"Msikae kimya wakati watu wasio wataalamu wanatoa taarifa zisizo sahihi. Elimu mliyoipata inapaswa kuisaidia jamii na kuokoa maisha ya Watanzania," alisema akitaja majukwaa ya kidijitali kama TikTok, Instagram na Facebook.