Tanzania yatakiwa kuandaa wataalamu zaidi wa afya
Afisa Mtendaji Mkuu Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Ellen Mkondya-Senkoro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, baada ya kumaliza kuzungumza katika mkutano wa tatu wa rasilimali watu sekta ya afya.
Muktasari:
- Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe, amesema nchi zote 11 wanachama wa jumuiya hiyo zinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya.
Dar es Salaam. Wadau wa sekta ya afya wameitaka Tanzania kubadili mkakati wa kuandaa rasilimali watu katika sekta hiyo kwa kuwekeza kwa vijana, ubunifu, teknolojia na huduma za kinga ili kukidhi mahitaji ya huduma za afya yanayotarajiwa kuongezeka kutokana na ongezeko la watu.
Wito huo umetolewa leo Jumanne, Julai 14, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa tatu wa rasilimali watu wa sekta ya afya (Human Resources for Health Conference) ulioandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF).
Viongozi na wataalamu wa afya wamesisitiza umuhimu wa kuweka mipango ya muda mrefu ya Tanzania kuwa na wataalamu wenye ujuzi na mifumo imara ya kutoa huduma bora za afya miongo ijayo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Ellen Mkondya-Senkoro, amesema mustakabali wa mfumo wa afya nchini utategemea uamuzi unaofanywa sasa kuhusu elimu, ukuzaji wa viongozi, sayansi na teknolojia.
Amesema makadirio yanaonyesha idadi ya watu nchini inaweza kufikia zaidi ya milioni 120 ifikapo mwaka 2050, hali inayobeba fursa na changamoto kwa wakati mmoja.
“Swali si kama tuna vijana wa kutosha ni kama tunawaandaa vijana hao kwa kuwapa ujuzi, afya na fursa wanazohitaji ili wachangie maendeleo ya Taifa,” amesema.
Ameonya Tanzania inapaswa kuhakikisha ongezeko la watu linakuwa mtaji wa maendeleo badala ya kuwa mzigo.
Amesema idadi kubwa ya vijana inaweza kuwa chachu ya ubunifu, uzalishaji na ustawi ikiwa watakuwa na afya bora, elimu, ujuzi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Dk Mkondya-Senkoro amesema ni wakati wa kubadili mtazamo wa upangaji wa rasilimali watu kwa afya kwa kuacha kuangalia idadi ya wahudumu pekee na kuanza kujiuliza aina ya wataalamu wanaohitajika katika siku zijazo.
Amesema wataalamu wa afya wa baadaye watahitaji ujuzi unaovuka mafunzo ya kawaida ya kitabibu, ukiwamo matumizi ya afya kidijitali, akili mnemba (AI), usimamizi wa takwimu za afya, uhandisi wa vifaa tiba, afya na mabadiliko ya tabianchi pamoja na huduma kwa wazee.
“Tanzania inabadilika. Miji inaongezeka, teknolojia inabadilisha utoaji wa huduma za afya, magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka na idadi ya wazee inaongezeka, lazima tuwaandae vijana kwa mazingira hayo,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kujenga viongozi ndani ya sekta ya afya akisema ujuzi wa kitaalamu pekee hautoshi kuleta mageuzi.
Amewataka wataalamu wenye uzoefu kuwalea na kuwapa nafasi vijana ili waweze kujifunza na kuongoza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Dk Mpoki Ulisubisya, amesema ni muhimu kuongeza uwekezaji katika huduma za kinga ili kupunguza msongamano wa wagonjwa hospitalini.
Ameeleza kuwa ongezeko la watu na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza vinahitaji mfumo wa afya unaozingatia zaidi kuzuia kuliko kutibu.
“Hakuna nchi iliyofanikiwa kutatua changamoto za afya kwa kutegemea huduma za tiba pekee, tuongeze uwekezaji katika kinga, watu wachache zaidi wataugua,” amesema.
Amesema ushiriki wa jamii umeonyesha mafanikio katika kuboresha afya ya mama na mtoto na unapaswa kuendelea kupewa kipaumbele.
Pia amesisitiza umuhimu wa usawa katika upatikanaji wa huduma za afya akisema ubora wa huduma haupaswi kutegemea eneo analoishi mwananchi.
“Dawa, vifaatiba, teknolojia na miundombinu inayopatikana Dar es Salaam inapaswa pia kupatikana Namtumbo, Tunduru na maeneo mengine nchini. Tunawatibu binadamu wale wale,” amesema.
Akizungumzia matumizi ya teknolojia, Dk Ulisubisya amesema akili unde inaweza kuongeza ufanisi wa wahudumu wa afya lakini haiwezi kuchukua nafasi ya utu na uwezo wa kuelewa mahitaji ya mgonjwa.
Wataalamu wa afya pia wametaka mfumo wa elimu uendane na mahitaji halisi ya soko la ajira ili kuepuka kuzalisha wahitimu wasiokuwa na ujuzi unaohitajika katika sekta hiyo.
Dk Julietha Tibyesiga kutoka Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo, amesema madaktari wengi wanaohitimu huingia kazini wakiwa na matarajio yaliyojengwa katika hospitali kubwa, lakini hukutana na mazingira tofauti wanapopangiwa vituo vya afya na hospitali za wilaya.
Amependekeza maboresho katika elimu ya udaktari ili kuongeza mafunzo kuhusu kinga, afya ya jamii na changamoto halisi zinazowakabili wahudumu katika maeneo ya vijijini.
“Elimu ya udaktari inapaswa kuwaandaa wahitimu kufanya kazi katika maeneo wanayotarajiwa kuhudumu, si katika hospitali za rufaa pekee,” amesema.
Aidha, amesema mfumo wa ulezi (mentorship) ni muhimu katika kuwaandaa viongozi wa baadaye wa sekta ya afya, akiwataka wataalamu wenye uzoefu kuwapa vijana mwongozo, nafasi za kujifunza na majukumu ya uongozi mapema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe, amesema nchi zote 11 wanachama wa jumuiya hiyo zinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya.
Amesema ukanda huo una upungufu wa wastani wa asilimia 46 ya rasilimali watu katika sekta ya afya, jambo linalohitaji ushirikiano na ubunifu ili kuziba pengo hilo.