Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi Viongozi wamwonavyo Hayati Mkapa

Jinsi Viongozi wamwonavyo Hayati Mkapa

Muktasari:

  • Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania wameeleza wanavyomkumbuka Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, ambaye ametimiza mwaka mmoja tangu alipofariki dunia Julai 24, 2020.

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania wameeleza wanavyomkumbuka Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, ambaye ametimiza mwaka mmoja tangu alipofariki dunia Julai 24, 2020.

Taasisi ya Benjamin Mkapa juzi iliandaa kongamano la kumbukumbu ya Mkapa kwa kutambua mchango wake, hasa kupitia taasisi hiyo, ambayo inatoa huduma za afya katika maeneo mbalimbali ya pembezoni hapa nchini.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Spika mstaafu, Anne Makinda na Balozi Ombeni Sefue, katibu mkuu kiongozi mstaafu.

Pia, viongozi wastaafu kutoka mataifa mbalimbali walishiriki kongamano hilo kwa njia ya mtandao na kumzungumzia Mkapa jinsi walivyomfahamu na kufanya naye kazi.

Viongozi hao ni Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza, Tony Blair, Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton, Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano.

Viongozi hao walimwelezea Hayati Mkapa kama kiongozi mzalendo ambaye alijitoa kusaidia wananchi maskini, aliyeamini katika kujenga taasisi na mwanaumajumui wa Afrika ambaye alishirikiana kwa karibu na jumuiya ya kimataifa.


Alichosema Rais Samia

Rais Samia alimwelezea Mkapa kama kiongozi aliyekuwa na maarifa mengi na wakati wa uongozi wake alisimamia mageuzi ya kiuchumi kwa kukaribisha wawekezaji kutoka nje, ambao walisaidia kujenga uchumi wa Taifa.

Alisema Mkapa alitumia uwezo wake wa diplomasia kuzishawishi taasisi za kifedha za kimataifa na nchi wahisani na kufanikiwa kupunguza deni la taifa karibu nusu kutoka asilimia 143.7 ya Pato la Taifa mwaka 1995 hadi asilimia 60.7 mwaka 2005.

“Miongoni mwa hatua kubwa alizochukua ni kutoa fursa kubwa kwa sekta binafsi na kukaribisha uwekezaji kutoka nje. Hatua hizi zilisaidia kuongeza mapato ya Serikali kutoka Sh331.2 bilioni mwaka 1995 hadi kufikia Sh2 trilioni mwaka 2005,” alisema Rais Samia.

Kiongozi huyo alisema Mkapa alianzisha taasisi nyingi hapa nchini, ikiwemo Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wakala wa Barabara (Tanroads), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na nyingine za kupambana na umaskini za Tasaf, Mkurabita na Mkukuta.

Alisema mchango wake haukuishia Tanzania, bali alishiriki katika masuala ya kimataifa, ikiwemo kuifufua Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuanzisha Umoja wa Afrika (AU) kutoka iliyokuwa OAU na pia katika utatuzi wa mgogoro wa Burundi.

“Baada ya kukabidhi uenyekiti wa Sadc mwaka 2004 pale Gaborone, Botswana baada ya kuona wahisani wanasuasua, Mzee Mkapa alitoa wazo la nchi wanachama kutoa michango kuanza ujenzi wa ofisi hiyo, naye alitangaza kwamba Tanzania itachangia Dola 500,000,” alisema.

Rais Samia alisimulia kwamba baada ya machafuko ya mwaka 2001 yaliyotokea Zanzibar, Mkapa aliunda jopo la viongozi mbalimbali yeye akiwa mmoja wao, ambalo lilikwenda nchi mbalimbali kueleza kilichotokea nchini.

“Katika kuifanya kazi hiyo nilijifunza mambo mengi ya siasa na diplomasia pamoja na hekima ambayo wakuu wa nchi wanapaswa kutumia kunapotokea changamoto hasa za kisiasa.

“Hatua hiyo ndiyo iliyoleta mwafaka wa kisiasa Zanzibar na nchi kwa ujumla kuendelea na shughuli zake bila vikwazo vya ndani wala nje,” alisema.


Kauli ya Kikwete

Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alisema alifahamiana na Mkapa kwa zaidi ya miongo minne na alifanya naye kazi kwa karibu kabla na baada ya kuwa Rais wa taifa hili kuanzia wakiwa wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM miaka ya 1980.

Alisema baadaye walikutana tena katika Baraza la Mawaziri wakati wa utawala wa Rais Mwinyi na alipotangaza nia ya kuwania urais, Mkapa alimpa ushirikiano wa kutosha bila masharti yoyote.

“Mkapa alikuwa mtu imara, wakati mwingine alikuwa mkali maana wakati mwingine unalazimika kufanya jambo,” alisema Kikwete na kuongeza kwamba, “alikuwa Mwanaumajumui wa Afrika aliyeipenda nchi yake.’

Kikwete alizungumzia pia Taasisi ya Benjamin Mkapa akisema ilianzishwa Aprili 2006 wakati wa utawala wake na ilisaidia juhudi za Serikali katika kufikisha huduma za afya kwa wananchi, hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema wakati wa utawala wake kulikuwa na changamoto ya uhaba wa wataalamu wa afya, hasa vijijini, licha ya kwamba Serikali ilikuwa na uwezo wa kuwalipa mishahara, hivyo Taasisi ya Benjamin Mkapa ilifanya kazi kubwa ya kupeleka wataalamu hao na kuwafanya watulie kwenye vituo vyao.

“Changamoto kubwa ilikuwa ni kuwafanya wataalamu wa afya wakae kwenye vituo vyao vya kazi huko vijijini. Wengi ilikuwa wakipelekwa, mtu anaangalia mazingira, anasema ngoja nikajipange, harudi tena,” alisema Kikwete.


Balozi Sefue

Kwa upande wake, Balozi Sefue alimwelezea Mkapa kama kiongozi aliyependa kusoma vitabu na majarida mbalimbali na alipenda kuonyesha njia ili wengine wafuate.

Sefue ambaye alikuwa msaidizi wake katika miaka 10 ya utawala wake, alisema Mkapa hakuwa mtu wa kujikweza, alikataa kuitwa “Mtukufu” na picha yake kuwekwa kwenye noti za Tanzania.

“Alikuwa Mkatoliki wa kweli, alihudhuria Misa Takatifu kila Jumapili. Alifanya kazi kwa bidii hata alipokuwa mgonjwa, nakumbuka alipokuwa hospitali huko Zurich, Uswis, alitoa hotuba yake ya kila mwezi kama utaratibu aliojiwekea,” alisema Balozi Sefue.

Aliongeza kuwa Mkapa aliamini katika falsafa ya ukweli na uwazi, alichukia rushwa na alianzisha taasisi mbalimbali akiamini kwamba uwepo wa taasisi imara ndiyo msingi wa uongozi bora katika Taifa.


Aliyosema Clinton

Rais mstaafu wa Marekani, Clinton alitoa pole kwa Rais Samia kwa kuwapoteza viongozi wawili ndani ya kipindi kifupi ambao ni Hayati Mkapa na Hayati John Magufuli.

Alisema Serikali yake na Hayati Mkapa walifanya kazi ya kuimarisha mifumo ya huduma za afya, ikiwemo kuanzisha maabara za kupimia maambukizi ya virusi vya Ukimwi

“Dira, jitihada na uongozi wa Rais Mkapa vinaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na mpango maalumu unaoongozwa na Serikali. Naipongeza Serikali kwa jitihada hizo,” alisema.

Aliongeza kuwa Mkapa aliwekeza nguvu katika kuongeza rasilimali watu katika sekta ya afya ili kupunguza uhaba wa wataalamu wa afya. Alisema alianzisha mpango ambao ulilenga kupeleka wataalamu wa afya na kuwafanya wabakie kwenye maeneo yao.

Kauli ya Blair

Kwa upande wake, Blair alisema baada ya kuondoka madarakani, Mkapa alianzisha Taasisi ya Benjamin Mkapa ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi na kuongeza nguvu katika mpango wa afya kwa wote.

“Nilipokuwa madarakani nilifanya naye kazi, nilimwona kama kiongozi wa pekee, mzalendo wa kweli, kiongozi na binadamu mwenye moyo safi. Yeye amekwenda lakini urithi aliouacha utaendelea kuishi,” alisema Blair.


Taasisi yenyewe

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Ellen Mkondya Senkoro alisema tangu kuanzishwa kwake taasisi hiyo miaka 15 iliyopita, imeweza kugusa maisha ya watu zaidi ya milioni 20, hasa waishio vijijini.

Alisema taasisi hiyo imeajiri wataalamu wa afya 9,000 katika kipindi hicho na kuifanya kuwa asasi ya kiraia iliyoajiri wafanyakazi wengi katika sekta ya afya baada ya Serikali.

Vilevile, alisema Taasisi hiyo imejenga na kukarabati vituo vya afya 537 nchi nzima na kuwezesha wananchi wengi kuzifikia huduma za afya katika maeneo yao.