Profesa Jay aruhusiwa kutoka hospitali

Muktasari:

  • Mkongwe wa Hiphop na mbunge wa zamani wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kwa jina la Profesa Jay, jana ameruhusiwa kutoka hospitali baada ya kulazwa kwa siku 127 akifanyiwa matibabu.


Dar es Salaam. Mkongwe wa Hiphop na mbunge wa zamani wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kwa jina la Profesa Jay, jana ameruhusiwa kutoka hospitali baada ya kulazwa kwa siku 127 akifanyiwa matibabu.

Profesa Jay alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam akipatiwa matibabu ya figo tangu Februari Mosi, 2022.

Taarifa iliyotolewa leo Juni 10, 2022 na hospitali hiyo imeeleza kuwa mwanamuziki huyo alipatiwa matibabu kwa takribani siku 127 na sasa ameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.

“Msanii Joseph Haule (Prof. J) jana ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupatiwa matibabu kwa siku 127 na afya yake kuimarika” imeeleza taarifa hiyo.

Nguli huyo wa muziki nchini, aliyejitosa katika siasa na kuwa mbunge wa Mikumi katika uchaguzi wa mwaka 2015 kupitia chama cha Chadema, ni miongoni mwa wasanii wachache waliowahi kuingia katika siasa nchini.

Kabla ya kuugua Profesa Jay alitamba na kibao cha ‘Utaniambia nini’ alichokitoa mwanzoni mwa 2022 ikiwa ni miaka miwili baada ya kumaliza muda wa ubunge wake.

Katika maisha yake ya muziki, Profesa Jay ametamba zaidi na kibao cha ‘Zali la Mentali’.