Profesa Kabudi aomba reli zote zipite Kilosa

New Content Item (2)

Muktasari:

  • Mbunge wa Kilosa ameomba Serikali kufufua Reli ya Kilosa-Kidatu ili kusaidia kukuza uchumi wa mji huo na vitongoji vyake.

Dodoma. Mbunge wa Kilosa (CCM) Profesa Palamagamba Kabudi ameiomba Serikali kuifufua reli kutoka Kilosa hadi Kidatu kwa kuifanyia ukarabati ili iweze kutoa huduma.

Profesa Kabudi amezungumzia mji wa Kilosa kuwa ni habu ya uchumi ikiwa Serikali itaamua kufanya hivyo kwani ni eneo pekee ambalo litakuwa likipitia na muunganiko wa reli tatu ikiwemo ya SGR, Tazara na MGR (Reli ya Kati).

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema Serikali kwa vipindi tofauti imeendelea kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Kuhusu ufufuaji wa reli kutoka Kilosa hadi Kidatu, amesema Serikali kupitia TRC katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 imetenga jumla ya Sh3.42 bilioni kwa ajili ya kuanza kazi za awali za marekebisho na ufufuaji wa njia katika kipande hiki chenye urefu wa kilomita 108 ambayo imefungwa kwa muda mrefu.

“Reli hii inaunganisha Reli ya kati na Tazara eneo la Kidatu, aidha kwa sasa TRC imekamilisha tathmini ya kihandisi ikiwemo makadirio ya gharama ya mradi  (Engineering estimate) na inaendelea na ukamilishaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumwajiri mkandarasi,”amesema Kihenzile.

Naibu Waziri amemuomba Profesa Kabudi kumsaidia ili pamoja na wananchi wa Kilosa kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na juhudi ya urejeshwaji wa njia hii ambayo ni muhimu kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo na abiria.

Amesema lengo la Serikali ni kuendelea kufanya maboresho katika maeneo yenye mahitaji ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma za usafiri na usafirishaji.