Profesa Mbarawa aridhishwa na ujenzi uwanja wa ndege Iringa
Muktasari:
- Uwanja huo wenye urefu urefu wa kilometa 2.2 na upana wa mita 31 na kugharimu kiasi cha Sh63.7 bilioni, unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.
Iringa. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameeleza kuridhishwa na kasi ya ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Iringam akisema utafungua fursa za kibiashara na Kanda ya Kusini utakamilika.
Uwanja huo utakaogharimu zaidi ya Sh63.7 bilioni ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayojengwa na Serikali kwa lengo la kufungua miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi ikiwemo sekta ya utalii.
Akizungumza leo Februari 15, 2023 baada ya kukagua ujenzi wa uwanja huo, Profesa Mbarawa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha uwanja huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
"Kiwanja hiki kitakuwa na taa na mnara wa kuongozea ndege wa muda, ila badaye utajengwa wa kudumu, hapo sasa wananchi watakuwa na fursa ya kusafiri mchana na usiku," amesema.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa barabara (Tanroads) Mkoa wa Iringa Mhandisi Daniel Kindole amesema
"Uwanja umekamilika kwa asilimia 45 kwa sasa bado tunafanya kuweka alama na michoro, kutakuwa na taa na ndege zitaweza kufanya kazi usiku na mchana," amesema Kindole
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Isimani, William Lukuvi ameishukuru serikali kwa ujenzi wa mradi huo na kusema utakapokamilika utakuza uchumi na kutoa ajira kwa vijana.
Awali akitoa salama za CCM na mjumbe wa Halmashauri kuu ya chama hicho Mkoa wa Iringa, Salim Abri amesema kuwa moja ya miradi inayofanyika Mkoani Iringa ni pamoja na uwanja huo.