Profesa Mkenda: Somo la ujasiriamali sasa ni lazima sekondari
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na walimu wa ajira mpya wa awali, msingi na sekondari (hawako pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa walimu hao yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo. Picha na Janeth Joseph
Rombo. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imeamua kuifanya biashara kuwa somo la lazima kwa wanafunzi wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, ikiwa ni sehemu ya mageuzi makubwa ya elimu nchini.
Akizungumza leo Julai 12, 2025 wakati wa kufungua mafunzo elekezi kwa walimu 133 wa ajira mpya wa shule za awali, msingi na sekondari katika Wilaya ya Rombo, Profesa Mkenda amesema lengo ni kuwajengea vijana misingi ya kujitegemea kupitia ujasiriamali.
“Kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne ni lazima vijana wafundishwe ujasiriamali. Kuna somo linaitwa biashara ni ujasiriamali na wote ni lazima wasome. Huwezi kulikwepa, ili hata ukimaliza shule, ukitaka kufanya shughuli zako, iwe rahisi,” amesema Profesa Mkenda.
Baadhi ya walimu wakiwa kwenye mafunzo elekezi ya walimu wa ajira mpya walioajiriwa katika utumishi wa umma mwaka 2024/25 katika Wilaya ya Rombo.
Amesema mageuzi hayo yanalenga kuwapa vijana ujuzi wa moja kwa moja na kwamba Serikali imeendelea kufanya tathmini na kupanua miundombinu ya elimu ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu hiyo unakuwa jumuishi na wa kisasa.
“Tumechakata, tumeangalia shule zilizopo na maeneo tunayoweza kuongeza madarasa. Shule za msingi sasa zinaweza kupokea wanafunzi wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, nchi nzima,” amesema Profesa Mkenda.
Amesisitiza kuwa, chini ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya elimu imepata msukumo mkubwa, hasa katika kuongeza shule na miundombinu ya kisasa ili kufanikisha mabadiliko ya mitaala na upatikanaji wa elimu kwa wote.
“Kuna shule za msingi lazima tujengee form one hadi form four. Tumeongeza sana sekondari nchi nzima. Uwekezaji katika elimu unaofanywa sasa unafurahisha kweli kweli,” amesema Profesa Mkenda.
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Rombo, Mwalimu Zema Jamal ameishukuru Serikali kwa kutoa ajira mpya 133 kwa walimu katika wilaya hiyo, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza uhaba wa walimu na kuongeza tija ya ufundishaji.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia ajira hizi mpya ambazo zitasaidia kuweka msawazo wa ikama ya walimu wa shule za msingi na sekondari. Hii itaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa walimu,” amesema Mwalimu Zema.
Aidha, amesema elimu endelevu kwa walimu imechangia kupunguza mashauri ya kinidhamu na kuongeza uwajibikaji, hatua iliyorejesha heshima ya walimu katika jamii.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, walimu 1,072 walipandishwa madaraja, 69 wakabadilishiwa muundo wa ajira na 45 wakapewa madaraja ya mserereko, hatua ambayo imeongeza ari ya utendaji kazi miongoni mwa walimu.