Profesa Ndakidemi awapa mbinu vijana, wanawake kujikwamua kiuchumi

Muktasari:

Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amewataka vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri, ili kuanzisha miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi.

Moshi. Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amewataka vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri, ili kuanzisha miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi.

Profesa Ndakidemi ametoa rai hiyo wakati akizungumza kwenye kongamano la wafanyabiashara na wajasiriamali lililoandaliwa na Diwani wa Kata ya Uru Kusini, Wilhad Kitaly lililokuwa na lengo la kushirikishana maarifa na kutoa elimu kuhusu fursa mbalimbali za biashara.

Amesema kila halmashauri hutoa asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, hivyo ni vyema makundi hayo yakahakikisha yanatumia fursa hiyo vizuri ili kujikwamua kiuchumi na kuyafikia malengo ya serikali.

"Ndugu zangu vijana, ipo mikopo ya halmashsuri isiyo na riba kwa ajili yenu, jiungeni kwenye vikundi sasa ili muweze kunufaika na mikopo hii na kuanzisha miradi ya kiuchumi, nendeni halmashauri watawapa maelekezo na elimu, msikubali kukaa vijiweni mkilia hakuna kazi" amesema.

Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Willy Machumu amesema vijana wanapaswa kutambua kuwa hali ya maisha siyo rahisi kama wanavyofikiria, hivyo amewataka kuongeza juhudi katika kufanya kazi, kujituma na kubuni miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Uru Kusini, Wilhad Kitaly amewashauri vijana kutochagua kazi za kufanya na kujitahidi kubadili changamoto kuwa fursa, ili kuweza kujipambanua zaidi katika kupambana na uhaba wa ajira.