Profesa Saffari ataja sababu kuacha siasa, aeleza alivyotimuliwa kazi kwa kumtetea Lipumba

Profesa Abdallah Saffari

Muktasari:

  • Profesa Abdallah Saffari aliyewahi kuwa kada na mshauri wa masuala muhimu ya kisheria wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chadema amesema akijitosa katika siasa hivi sasa atakuwa amejitoa kafala, ndiyo maana amejiondoa huko akidai hakuna watu makini.

Dar es Salaam. Katika siasa za Tanzania, jina la Profesa Abdallah Saffari si ngeni masikioni mwa watu, amekuwa mmoja wa wasomi waliojitokeza kwenye siasa, hasa za upinzani, akilenga kuleta mabadiliko ya kimfumo na kiutawala hapa nchini.

Licha ya kubobea kwenye masuala ya sheria na kusaidia watu kwenye eneo hilo, Profesa Saffari aliingia pia kwenye siasa akiwa na msimamo thabiti wa kusimamia ukweli, hata hivyo baadaye aliamua kuachana na njia hiyo kutokana na kinachoendelea huko.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Profesa Saffari nyumbani kwake Dar es Salaam ambapo ameeleza sababu za kuachana na siasa na sasa amejikita kwenye utunzi wa vitabu kama njia nyingine ya kuendeleza harakati zake za ukombozi.

Profesa Saffari aliyewahi kuwa kada na mshauri wa masuala ya kisheria wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chadema, anasema akijitosa katika siasa hivi sasa atakuwa amejitoa kafala, ndiyo maana amejiondoa huko akidai hakuna watu makini.

Nguli huyo wa sheria nchini anasema hajaona mtu anayemvutia kwenye siasa kwa sasa kama ilivyokuwa huko nyuma. Anasema zamani alivutiwa na watu kama Bob Makani 9Mwenyekiti wa pili wa Chadema), Hayati Julius Nyerere (Rais wa kwanza wa Tanganyika), Edward Sokoine (aliyekuwa Waziri Mkuu), Kingunge Ngombale Mwiru na mwanasiasa wa tangu enzi za Tanu, Joseph Kasalla-Bantu.

“Hawa watu hawapo hivi sasa, lakini kuna watu waliwaangusha, hivyo najua na mimi nitaangushwa, ndio maana nimeamua kujikalia kimya na kuandika vitabu vyangu ili kuacha alama ya uandishi.

“Sasa mtu atanifuata ataniambia nini? Si ninaandika vitabu vyangu, kama unataka vichape au basi, sitaki kugombana na Serikali, nitajiumiza bure maana nasimamia ukweli, lakini watu hawataki ukweli, badala yake wanadanganyana, siwezi kuwa ‘chawa’.

“Utu uzima huu, niwe chawa mzee kwa kusema uongo? Haipendezi kabisa… nimejikalia zangu kimya, nafanya shughuli zangu za uandishi wa vitabu,” anasema Profesa Saffari aliyewahi kuwa wakili mkuu mwandamkizi wa Serikali.

Uchawa ni hali ya mtu au kundi fulani cha watu, kwa sababu ya masilahi binafsi au ya kisiasa, kusifia jambo au kuunga mkono uamuzi fulani hata kama unaumiza mtu au nchi.

Profesa Saffari ambaye anaonekana mtu mwenye msimamo mkali, anasema hivi sasa ukiwa mkweli utagombana na makundi mbalimbali, badala yake watu wanataka maisha rahisi ambayo yeye hawezi kuyafanya hivyo.

“Mimi ni mkweli sana, naogopa nikienda kwenye mambo mengine (siasa), nitagombana, hata nikienda katika upinzani nitagombana sana. Katika maisha, kila mmoja ana kipawa alichojaaliwa na Mungu.

“Mimi naweza kuandika, tena kwa weledi, umakini na ufasaha bila matatizo, sasa hiki kitu Mungu amenijalia,” anasema Profesa Saffari aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara).


Utunzi wa vitabu

Pamoja na mambo mengine ya kitaalamu aliyobarikiwa, Profesa Saffari ni mtaalamu wa uandishi wa vitabu, anasema miongoni mwa vitabu maarufu alivyoviandika ni pamoja na kitabu cha “Mashtaka ya Jinai na Utetezi” kinachotumika katika vyuo vikuu na Shule Kuu ya Sheria kufundishia mwenendo wa mashtaka ya jinai.

Mbali na hilo, Profesa Saffari anasema ameandika kitabu cha “Harusi” ambacho kimetumika kama rejea katika shule za sekondari nchini, pia riwaya za “Kabwela” cha mwaka 1978, “Joka la Mdimu” na “Piga Bongo”.

Pia, Profesa Saffari ameandika kitabu cha “Nahau za Kiswahili” na hivi sasa yupo mbioni kumaliza vitabu vingine kikiwemo cha hadithi ya “Mzuka wa Tito” alichoshirikiana na mwanaye, Mariamu na kitabu kingine cha “Safari ya Uwakili” kinachozungumzia maisha yake ya uwakili.

“Katika vitabu hivi, ‘Joka la Ndimu’ kimenipatia mafanikio makubwa ikiwemo fedha za kutosha (hakuzitaja), kwa sababu kimetumika katika shule zote za sekondari. Kingine ni kitabu cha ‘Harusi’ kinachotumika vyuo vikuu na shule za sekondari,” anasema Profesa Saffari ambaye aliwahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Hata hivyo, Profesa Saffari aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Masomo na Mipango wa Chuo cha Diplomasia, anasema hivi sasa utamaduni wa Watanzania kusoma vitabu umepungua na kwamba kama una vitabu vyako havitumiki katika taasisi za elimu, vyuo vikuu au shule, basi huwezi kuviuza.

Profesa Saffari aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu vya Fasihi Tanzania (Uwavita) kati ya mwaka 1999 hadi 2000, anasema kuanzia miaka 1960 hadi 1980 kulikuwa na mwamko wa Watanzania kusoma vitabu.

Anasema kitabu cha “Joka la Mdimu” kinatokana na ukweli, akieleza kuwa wakati akiwa Wakili wa Serikali, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilikuwa ni ofisi ndogo, watu waliiunguza na moto na wakati wa Sokoine kulikuwa na changamoto ya mambo ya ufisadi.

“Ofisi yangu ilikuwa jirani na Ofisi ya Mama Malecela (mke wa John Malecela), wakati BoT inaungua tulikuwa nao, nikasema lazima kutakuwa na watu wanahusika, nikatunga kitabu cha ‘Joka la Mdimu’ kuakisi uwezekano wa mafisadi walioichoma benki,” anasema Profesa Saffari.


Taaluma ya sheria

Profesa Saffari anasema anajisikia vibaya kuona baadhi ya wanafunzi waliopita mikononi mwake wakifanya mambo kinyume cha utaratibu wa fani zao.

“Nasikitika sana kuona wakiwa hivyo, tena nimewafundisha mwenyewe na baadhi yao wamekosa umahiri. Hawa nimewaelezea vizuri pia katika kitabu changu cha safari ya uwakili, chenye sura 16 kinachozungumzia maisha yangu ya uwakili wa Serikali na kesi kubwa nilizosimamia na hali iliyokuwa miaka hiyo na sasa,” anasema.

“Miongoni mwa kesi ngumu nilizowahi kuzifanya na kuziandika katika kitabu changu ni kesi ya uchaguzi wa Igunga (Tabora) kati ya Joseph Kashinde (Chadema) na Dk Dalaly Kafumu (CCM), hii kesi tulishinda lakini Mahakama kuna kitu ilifanya. Kesi hii ilinikera, nikataka kuacha uwakili,” anasema Profesa Saffari bila kufafanua zaidi.

Pia, nasema wakati akihudumu katika Chuo cha Diplomasia, kulitokea kesi kubwa ya rushwa iliyowahusisha marais wawili wa kigeni mjini Arusha, ambapo Rais awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa alimtaka kushiriki katika kesi hiyo kuwa mwendesha mashtaka.

“Alinifuata Dk Edward Hosea ambaye ni mwanafunzi wangu, akaniambia mwalimu Serikali inataka ‘second opinion’, nilivyosoma makabrasha nikasema mbona kuna ushahidi wa kutosha, ndipo Mkapa akaniteua mimi na mwenzangu, Profesa Zabron Gondwe kuwa waendesha mashtaka maalumu.

“Inapotokea Serikali ina hofu na watendaji wake wa ndani, basi inateua waendesha mashtaka maalumu wa nje katika Ofisi ya DPP, hii kesi ilikuwa ngumu chupuchupu kufariki dunia kwa sababu nilikuwa mtu wa kuwa mwendesha mashtaka maalumu kusimamia kesi katika historia ya Tanzania, lakini wahusika walifungwa,” anasema Profesa Saffari.

Mbali na hilo, Profesa Saffari anasema kesi nyingine iliyovuta hisia za Watanzania ya kina Abubakari Mwilima na wenzake, waliomfuata ofisini na kwenda kuishtaki Serikali iliyoruhusu Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania) iwe taasisi ya dini hiyo, lakini wenyewe walidai sio taasisi.

“Walishtaki Bakwata kuwa sio taasisi ya Kiislamu, siku ya kuandika hukumu kwa Jaji Ruhekelo Kyando, umati wa watu ulikuwa mkubwa kuanzia ilipokuwa Mahakama ya Rufani, Wizara ya Ardhi hadi baharini. Katika maisha yangu sikuwahi kuona watu wengi wanakuja mahakamani namna ile.

“Baada ya hukumu ile, Jaji Kyando akafariki dunia katika mazingira ya ajabu, mimi nikaumwa karibu siku tatu hata sijifahamu,” anasimulia.

Kesi nyingine, Profesa Saffari anasema ni mauji ya Magomeni Mwembechai ya mwaka 1999 wakati akiwatetea Sheikh Issa Ponda na mwenzake Mussa Kundecha walioshtakiwa kwa madai ya mauaji ya Mtunguja.

“Hii kesi ilikuwa balaa pale Kisutu (Mahakama Hakimu Mkazi) palikuwa kuna kila aina ya ulinzi) hii kitu kitabu changu cha Safari ya Uwakili kitasheheni haya mambo,”anasema Profesa Saffari.

Katika hatua nyingine, Profesa Saffari anasema mwaka 1999 alifukuzwa kazi serikalini kwa kosa la kumtetea Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake waliopitisha muda katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mbagala Zakhiem.

“Profesa Lipumba alipigwa hadi kuvunjwa mkono, sasa mimi nilimtetea mahakamani jambo lililosababisha kutimuliwa serikalini,” anasema Profesa Saffari.