Profesa Shemdoe wanasayansi kuhamasisha matumizi ya mbegu bora

Muktasari:

  • Wataalamu wa kilimo nchini wametakiwa kutumia taaluma walizonazo kuhamasisha wakulima kutumia mbegu zilizo thibitisha na Mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu ili kuondokana na   changamoto ya wakulima waliowengi  kutumia mbegu zisizo na ubora.


Dodoma. Wataalamu wa kilimo nchini wametakiwa kutumia taaluma walizonazo kuhamasisha wakulima kutumia mbegu zilizo thibitisha na Mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu ili kuondokana na  changamoto ya wakulima waliowengi  kutumia mbegu zisizo na ubora.

Hayo yamesemwa Alhamis Septemba 22,2022, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi),  Profesa Riziki Shemdoe wakati akifungua mkutano wa mwaka wa umoja wa wanasayansi wa mazao na vipando Tanzania (CROSAT).

“Tanzania tunategemea kilimo. Mambo waliyojadili ni upatikanaji wa mbegu bora. Muangalie namna bora ya kuwahusisha watalaamu waliopo katika mamlaka za Serikali za mtaa katika umoja huu,”amesema.

Amesema katika mamlaka ya Serikali za mitaa, wanao maofisa ugani wasiopungua 7,000 ambao wakiwahusisha kuwa wanachama wanaweza kuwafikia wakulima kwa urahisi.

“Mamlaka nyingi za Serikali za Mitaa zinategemea kilimo, tutakapokuwa na mbegu nzuri tunaweza kupata mapato mengi na hivyo kuleta maendeleo,”amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu, Patrick Ngwediagi amewashauri Crosat kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi ya mbegu bora ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

Mwenyekiti wa CROSAT, Profesa Kalunde Sibuka amesema wamekuta ili kuboresha Katiba ya umoja wao na kuongeza tija katika kilimo cha mazao.

“Tumekutana kufahamiana, kupanga jinsi ya kuboresha Katiba yetu na kupanga mikakati kuendelea na shughuli zilizoainishwa katika Katiba,”amesema