Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Shivji atetea kizazi cha kidijitali, Udasa walilia uhuru wa mawazo

Muktasari:

  • Profesa Issa Shivji amesisitiza kuamini vijana na kubadili mbinu za uandishi na ufundishaji ili kuendana na ubunifu unaovutia usomaji wa kizazi kipya.

Dar es Salaam. Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Issa Shivji, amewataka wanazuoni na waandishi wa vitabu kubadili mbinu za kufundisha na kuandika ili kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa.

Wakati Profesa Shivji akisema hayo, Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) wamesema wanazuoni wanahitaji kuwa na uhuru wa mawazo bila woga, na watasimamia msingi huo kwa mujibu wa katiba ya umoja huo ya mwaka 2016.

Profesa Shivji amebainisha hayo katika uzinduzi wa kitabu chake kipya kiitwacho “Barua kwa mpendwa Azimio”, kilichozinduliwa jana, Jumanne, Juni 16, 2026, chuoni hapo na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwemo wanazuoni wenzake.

Maprofesa Issa Shivji na Penina Mhando, wakiendesha mjadala wa uzinduzi wa kitabu cha Mpendwa Azimio, kilichoandikwa na Profesa Shivji, jijini Dar es Salaam, June 16, 2026.

Amesema wanataaluma wamezoea kuandika makala na vitabu virefu vya kitaaluma, wakati vijana wa sasa wanapata taarifa kwa haraka kupitia majukwaa ya kidijitali.

Mwanazuoni huyo amesema hali hiyo imewafanya vijana kuacha kupenda kusoma vitabu, na hivyo kukosa maarifa muhimu ambayo yangewasaidia kukuza uelewa wao katika masuala mbalimbali.

“Changamoto kubwa iliyopo si vijana kukosa hamasa ya kujifunza, bali ni mbinu zinazotumika kuwafikishia maarifa hayo. Wanataaluma tunaandika makala za kurasa 25, wakati vijana wanapata majibu mtandaoni kwa muda mfupi. Lazima tubadili mbinu,” amesema.

Vijana ni kundi la watu waliopo katika kipindi cha mpito kati ya utoto na utu uzima. Kundi hili lina nguvu, ubunifu na uwezo mkubwa wa kujifunza kupitia njia mbalimbali za teknolojia mpya, hasa mitandao ya kijamii, ambapo hupata fursa ya kupata taarifa, kujifunza na kuwasiliana kwa urahisi.

Hata hivyo, matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yanatajwa kupunguza hamasa kwa vijana kusoma vitabu na maandiko marefu ya kitaaluma. Wengi hupendelea taarifa fupi, picha na video zinazopatikana kwa haraka, jambo linalopunguza hamasa ya kusoma maandiko yanayohitaji umakini na muda mrefu.


Mbinu mpya

Profesa Shivji, ambaye ni mbobezi wa sheria, ametolea mfano wa kitabu chake kipya akisema kimetumia mtindo wa kawaida wa uandishi kwa kutumia mbinu changamani zinazolenga kumfikia msomaji wa kizazi kipya.

Amesema ametumia barua, mazungumzo ya kifalsafa, simulizi na majibizano ya kufikirika ili kufanya maudhui kuwa rahisi, ya kuvutia na yasiyochosha.

Wanazuoni  Udsm wakipata maelezo kuhusu maudhui ya Kitabu kipya cha Profesa Issa Shivji, muda mfupi baada ya uzinduzi wa kitabu hicho jijini Dar es Salaam, June 16, 2026.

Kwa mujibu wake, lengo ni kuhakikisha maarifa mazito kuhusu historia, siasa na maendeleo yanawafikia vijana kwa lugha wanayoielewa na kuipokea kwa urahisi.

Amefafanua kuwa kitabu hicho, kilichopigwa chapa na Mkuki na Nyota Publishers na kuzinduliwa na Udasa, kimegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni “Barua kwa mpendwa Azimio”, kipengele kilichojengwa katika mtindo wa kifasihi unaokumbusha kazi za Shaaban Robert katika fikra ya “kusadikika”.

Ndani yake, Shivji ameandika jumla ya barua 15, ambapo barua 10 zimehusu awamu ya kwanza ya uongozi wa Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere, huku kila awamu ya baadaye ikipewa barua moja moja.

“Azimio la Arusha halipaswi kuonekana kama tukio la muda uliopita pekee, bali kama falsafa ya kudumu ya kujenga uchumi na jamii yenye usawa,” amefafanua.

Azimio la Arusha ni tamko la kisiasa na kiuchumi lililotangazwa Februari 5, 1967 katika mji wa Arusha na Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, likiweka msingi wa sera ya ujamaa na kujitegemea.

Azimio hilo lilichora ramani ya Tanzania ambayo ililenga kujenga jamii yenye usawa, kupunguza unyonyaji na kuimarisha maendeleo kupitia umiliki wa pamoja wa rasilimali muhimu.


Wito wa kuamini vijana

Katika maelezo yake, Profesa Shivji amesisitiza kuwa ni lazima jamii iache mtazamo wa kuwadharau vijana na badala yake iwaamini na kuwapa nafasi ya kujifunza kupitia njia zinazowafikia, ili wanufaike na elimu ya historia na falsafa za maendeleo kwa mbinu rahisi zinazogusa maisha yao badala ya kubaki kwenye maandishi mazito ya kitaaluma.

“Mimi bado ninawaamini vijana. Angalia hata Traoré na Sankara, ni vijana lakini wameaminiwa wamefanya vizuri,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhadhiri mwandamizi wa chuo hicho, Profesa Penina Mhando, amesema kuna pengo kubwa la uelewa wa historia miongoni mwa vijana wa sasa.

Ameeleza tukio alilowahi kulifanya akiwa Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu, na zaidi ya vijana 300 waliulizwa kuhusu Azimio la Arusha na falsafa ya ujamaa, lakini wengi hawakuweza kujibu.

Amesema hali hiyo inaonesha haja ya vitabu vinavyotumia lugha rahisi na mbinu bunifu ili kuziba pengo hilo la maarifa.


Udasa wataka uhuru wa kitaaluma

Mwenyekiti wa Udasa, Profesa Elgidius Ichumbaki, amesisitiza umuhimu wa wanazuoni kuwa huru kutoa mawazo yao bila hofu.

Profesa Issa Shivji, akionesha kitabu chake kipya muda mfupi baada ya kukizindua, June 16, 2026.

Profesa Ichumbaki amempongeza Profesa Shivji kwa kuandika kitabu hicho, akisisitiza uhuru wa kitaaluma kwa wanazuoni.

Amesema wanataaluma wanatakiwa kuwa huru kutoa maoni hasa katika kipindi ambacho jamii inakabiliwa na changamoto.

“Ni lazima tutumie taaluma zetu bila kujificha. Vitabu ni nyenzo ya kupinga matendo yanayotishia ustawi wa demokrasia nchini,” amesema.

Amesema wanataaluma wanapojifungia na kuogopa kutoa mawazo yao, wanalinyima taifa fursa ya kuzalisha viongozi wenye fikra fumbuzi.

“Dira yetu Udasa ni kuwa taasisi inayoaminiwa na watu. Katika katiba yetu ya 2016 inatuelekeza kulinda uhuru wa kitaaluma na kuhakikisha wajibu wa kitaaluma unatekelezwa ipasavyo,” amesema.

Amesema ushauri ambao umekuwa ukitolewa kwa wanazuoni kujiepusha na matamko ili kulinda uhuru wao, Udasa itaendelea kulinda uhuru wao na kukataa kuzuiwa ndani na nje ya chuo.

Amesema Udasa itaendelea kusimamia uadilifu wa kitaaluma ndani na nje ya UDSM, kukuza uaminifu na ushiriki wa wanajamii nchini.

“Tusiache kuuliza maswali magumu, tusiache kujifunza na kutoa maoni yetu kwa maslahi ya nchi yetu,” amesema.


Alichokisema Mabala

Aidha, uzinduzi wa kitabu hicho pia umeibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa elimu katika kizazi cha sasa.

Mwandishi mkongwe wa vitabu, Richard Mabala, amesema kufikia mabadiliko ya mifumo na jamii kupenda vitabu, yanahitajika mageuzi ya elimu.

Mwonekano wa Kitabu kipya cha Profesa Issa Shivji, kilichozinduliwa June 16, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema mfumo wa sasa wa elimu umewafanya wanufaika wa elimu kukariri maarifa badala ya kupenda kusoma na kudadisi maarifa, hali inayofanya kuwa na vijana wasiopenda kusoma vitabu.

“Tatizo kubwa ni mfumo mzima wa elimu. Mwanafunzi wa leo anaandaliwa kukariri maarifa badala ya kutafuta maarifa. Tunapaswa kujiuliza tunatokaje hapa watu wapende kusoma,” amesema.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuki Mgoya, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuki na Nyota Publishers, wachapishaji wa kitabu hicho, amesema kitabu si tu maandishi na karatasi zinazotumika, bali ni sauti ya mwandishi anayechangia maoni yake kwa jamii.

“Kitabu ni kumbukumbu isiyofutika, inayoenda kwenye kizazi kijacho, ikifikia jamii kubwa,” amesema.

Mkuki amerejea kitabu cha Shivji akisema kimelenga masuala ya uchumi, haki na matabaka ya watu kikiwa na mbinu ya kuzungumzia masuala mengi mazito kwa njia rahisi.

Amesema pia kimegusia uchumi, maendeleo, siasa na kukumbusha kuhusu nafasi ya ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo, haki zao na fursa wanazopata.

“Profesa Shivji anaandika bila woga, hafichi anapozungumza, sisi wachapishaji wake tunaungana naye. Hata muundo wake na jalada tumeliweka kwenye muundo utakaowavutia vijana,” amesema.

Amefichua kuwa kitabu hicho kinaibua mambo ya msingi yenye mchango kwa Taifa na Bara kwa ujumla, akisisitiza kuwa hakipaswi kubaki kwenye kabati bali kiifikie jamii, huku akisisitiza wanazuoni kuendelea kuandika vitabu kwa maslahi ya jamii na Taifa.