Puma Energy inavyochochea ajenda ya serikali ya nishati safi
Muktasari:
- Mradi huo unarajiwa kuleta mapinduzi ya nishati nchini, na kuchangia katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), hususan lengo namba 7 la upatikanaji wa nishati safi na nafuu kwa wote.
Morogoro. Katika kuunga mkono ajenda ya serikali ya kuhimiza matumizi ya nishati safi na endelevu, kampuni ya Puma Energy Tanzania imezindua rasmi kituo cha umeme wa jua chenye uwezo wa kilowati 570 katika kiwanda cha tumbaku cha Alliance One Tanzania Tobacco Limited (AOTTL) kilichopo Kingolwira, Morogoro.
Mradi huu ni sehemu ya juhudi za kitaifa kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyorekebishika na kuchochea maendeleo ya viwanda kupitia nishati rafiki kwa mazingira.
Uzinduzi huu unakuja wakati ambapo Serikali ya Tanzania kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) inasisitiza uwekezaji katika nishati mbadala ili kufanikisha uchumi wa viwanda unaojali mazingira.
Kituo hicho cha kisasa kimejengwa kwa kutumia paneli 1,296 za sola na inverter sita zenye ufanisi wa hali ya juu, kikitarajiwa kutoa umeme wa uhakika kwa kipindi chote cha uzalishaji wa kiwanda kuanzia Mei hadi Oktoba kila mwaka. Mfumo huu umeunganishwa na gridi ya taifa, na unatekelezwa kupitia Mkataba wa Ununuzi wa Umeme (PPA) wa miaka 10 kati ya Puma Energy na AOTTL.
Akizungumza leo Juni 9, 2025 wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah amesema mradi huo ni nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kijamii.
“Mradi huu ni mfano halisi wa utekelezaji wa dira ya taifa ya kuimarisha nishati safi kwa maendeleo ya viwanda. Tunaamini nishati safi si tu mbadala wa nishati ya kawaida, bali ni nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Tanzania ya viwanda.”
Mradi huu uliojengwa kwa kipindi cha mwezi mmoja tu, kuanzia Machi hadi Aprili 2025, ulianza rasmi kazi mnamo Mei 4, 2025, na unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za nishati kwa kiwanda cha AOTTL huku ukipunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Puma Energy, mfumo huo una dhamana ya utendaji wa miaka 30, hatua inayodhihirisha dhamira ya kampuni katika kusaidia uendelevu wa mazingira na kuhimiza ubunifu katika sekta ya nishati.
Mradi huu unakuja katika kipindi ambacho serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendeleza mikakati ya kupanua upatikanaji wa nishati safi, ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwekezaji binafsi katika teknolojia za sola, upepo, na vyanzo vingine mbadala.