Putin afichua silaha mpya za nyuklia

Muktasari:

  • Alisema silaha zilizoboreshwa zaidi ni pamoja na makombora mpya ya masafa marefu ambazo zinaweza kupachikwa vichwa vidogo vya nyuklia.

Kiongozi wa Urusi amefichua siri kuwa Taifa hilo lina silaha mpya za nyuklia ambazo amesema zinaweza kushambulia shabaha yoyote watakayolenga duniani huku kukiwa na nafasi ndogo ya kulizuia.

Katika hotuba yake kwa Taifa Alhamisi, Putin alitoa onyo kali kwamba mashambulizi yoyote dhidi ya Urusi au washirika wake yatajibiwa haraka na Urusi.

Wakati Putin akitoa hotuba hiyo, picha za video za silaha mpya zilikuwa zikionyeshwa nyuma yake katika ukumbi wa mkutano jijini Moscow, ambamo Putin alizungumza na wabunge.

Amesema silaha zilizoboreshwa zaidi ni pamoja na makombora mpya ya masafa marefu ambazo zinaweza kupachikwa vichwa vidogo vya nyuklia.

"Halipai juu sana, ni vigumu sana kulitambua likipita, lina uwezo wa kubeba kichwa cha nyuklia na linaweza kufika popote pale. Aidha, njia linayofuata haiwezi kutabirika na adui; linaweza kukwepa vizuizi na kimsingi haliwezi kuzuiwa na mifumo ya sasa ya kinga dhidi ya makombora na hata mifumo inayotarajiwa kuundwa siku zijazo," amesema.

Katika nusu ya kwanza ya hotuba hiyo yake kwa Taifa, ameahidi kupunguza viwango vya umaskini nchini humo.

Kisha, alionyesha mkusanyiko wa silaha mpya, likiwemo kombora alilodai linaweza kufika pahala popote duniani.

Putin ameelezea sera zake muhimu za muhula wa nne, Taifa hilo linapokaribia kufanya uchaguzi. Anakabiliwa na wapinzani saba, lakini hakuna mmoja kati ya hao anayetarajiwa kutoa ushindani mkubwa kwake.

Mpinzani wake mkuu Alexei Navalny hajafanyi kampeni kwa sababu amezuiwa kuwania urais na ametoa wito kwa wapiga kura wanaomuunga mkono kususia uchaguzi huo.

Aidha, Putin hakushiriki mdahalo wa wagombea uliorushwa moja kwa moja kwenye runinga Jumatano na kuwashirikisha wagombea hao wengine.