Radi yaua wanne wakichimba kaburi Chunya

Muktasari:

Watu wanne wamefariki dunia papo hapo na mwingine kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakati wakichimba kaburi katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Chunya. Watu wanne wamefariki dunia papo hapo na mwingine kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakati wakichimba kaburi katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Watu hao walipigwa na radi Jumapili Januari 9, 2022 wakichimba kaburi kwa ajili ya kumzika ndugu yao aliyefariki Januari 7.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya (DC), Mayeka Mayeka amethibitisha kutokea tukio hilo huku akiwataja waliofariki kuwa ni pamoja na Yohana James (30), Paul Mwasongole (40), Swalehe Ibrahim (23) wakazi wa Chunya mjini na Bonny Lauliano mkazi Mkoa wa Songwe.

Amesema kuwa Zuberi Mahona (40) ambaye ni mkazi wa Chunya mjini alijeruhiwa katika tukio hilo.

Amesema tukio hilo limetokea katika makaburi ya Kibaoni Chunya ambapo wakati wanachimba kaburi mvua iliyoambatana na radi ilianza kunyesha.

DC Mayeka amesema miili ya waliofariki imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Chunya huku majeruhi akiendelea vizuri na kuwataka wananchi watulie katika kipindi hiki cha maombolezo.

Shuhuda ambaye alikuwa kwenye eneo hilo la tukio, Meshack Luvanda amesema wenzao hao waliopigwa na radi wakiwa makaburini kutokana na mvua iliyoambatana na radi.

Amesema baada ya kupigwa radi Polisi walifika eneo la tukio na kubeba miili hadi hospitali ya Wilaya ya Chunya.