Radi yaua wawili Bukombe

Muktasari:

  • Mmoja aliyeuawa ametajwa kwa jina la Naomni Leli anayekadriwa kuwa na umri wa miaka 28 aliyekuwa akifua nguo bondeni akiwa ameweka mtoto wake pembeni na mtoto amebaki salama, huku mwingine aliyetajwa kwa jina la Mama Angelina alikuwa akichimba viazi na mwenzake shambani.

 Bukombe. Watu wawili wameuwawa kwa kupigwa na radi kwa nyakati tofauti mkoani Geita, akiwamo aliyekuwa akifua nguo mtoni, na mwingine aliyekuwa akichimba viazi sambani wakati mvua ikinyesha.

 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Msangila Kata ya Runzewe Magaribi, Emanuel Masanja amemataja Naomni Leli anayekadriwa kuwa na umri wa miaka 28 aliyekuwa akifua nguo bondeni akiwa ameweka mtoto wake pembeni na mtoto amebaki salama.

Amesema tukio hilo limetokea leo Alhamisi Septemba 28, 2023 majira ya saa 5:30 asubuhi wakati mvua iliyokuwa imeambatana na radi kali ikinyesha.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Namsega kata ya Runzewe Magaribi, Chiristopha Kasigwa amesema leo majira ya 6:30 mchana mama mmoja aliyetajwa kwa jina la Mama Angelina, amefariki duni kwa kupigwa na radi wakati akichimba viazi alivyokuwa amenunua kwenye shamba la Mzee Deus Ftali mkazi wa kijijini papo.

Shuhuda wa tukio hilo, mkazi wa Kata ya Uyovu, Mariamu Mihayo amesema walikwenda na marehemu kuchimba viazi kwenye shamba hilo.

"Tumetoka sote asubuhi nyumbani Kijiji cha Azimio kata ya Uyovu kuja kuchimba viazi, wakati mwezagu akichimba viazi ilianza kunyesha mvua nikamwambia twende kwa majirani tukajifiche, lakini yeye hakutoka.

“Baadaye mimi nikatoka kwenda kwenye mti wa mwembe shambani hapo, niliporudi baada ya mvua kukata nilimkuta ameaguka chali na amebabuliwa na radi," amesema Mariamu.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita, Sophia Jongo amesema bado hajapata taarifa hiyo.