Rafiki zake Majaliwa waomba nao wakumbukwe

Muktasari:
Majaliwa amejipatia umaarufu baada ya kujitosa na wenzake katika ajali ya ndege ya Precision iliyopata ajali wakati ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera, ambapo walifanikiwa kuokoa watu 24, huku wengine 19 wakifariki.
Bukoba. Wakati jina la Majaliwa Jackson, mchuuzi wa dagaa mwalo wa Nyamkazi Manispaa ya Bukoba ndilo likiendelea kuvuma, vijana watatu walioshirikiana naye wameibuka na kuomba kupewa mafunzo ya kuzamia na vifaa vya uokozi.
Majaliwa alijipatia umaarufu huo baada ya kujitosa na wenzake katika ajali ya ndege ya Precision iliyopata ajali wakati ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera, ambapo walifanikiwa kuokoa watu 24, huku wengine 19 wakifariki.
Akizungumza na Mwananchi Digital juzi Novemba 9, mmoja wa vijana hao, Sadam Sadath, mvuvi katika mwalo huo amewataja wenzake alioshirikiana nao pamoja na Majaliwa kufungua mlango wa ndege katika jitihada za kuokoa walikuwa ndani ya ndege kuwa ni Ally Athuman na Jost Festo ambao pia ni wavuvi katika mwalo wa Nyamkazi.
Amesema yeye, Majaliwa na wenzake wawili ndio walikuwa wa kwanza kufika eneo la ajali iliyotokea mjini Bukoba Novemba 6, mwaka huu wakitumia boti yao ya uvuvi.
Huku akiungwa mkono na mvuvi mwenzake, Ally Athman, Sadath anasema wakati ajali hiyo inatokea, yeye na wenzake pamoja na Majaliwa walikuwa mwalo wa Nyamkazi wakiendelea na shughuli zao za kila siku ndipo wakaona ndege ikitumbukia ziwani na kukimbia haraka eneo la ajali kutoa msaada.
Anasema kwa sababu Majaliwa ndiye aliketi eneo la mbele la mtumbwi, wenzake walimpa kasia ili autumie kupiga mlango katika jitihada za kuufungua huku wakishirikia kuuvuta kwa kutumia mkanda ndipo mlango ulipofunguka ghafla na kumbamiza Majaliwa kwenye paki la uso hadi kuzimia na kukimbizwa hospitali sambamba na majeruhi wengine wa ajali ya ndege waliokolewa.
Akijibu swali la kwa nini wao hawakutajwa, huku sifa zote akipewa Majaliwa wakati walishirikiana wote, Sadath anasema hilo limetokana na Majaliwa kujeruhiwa hadi kulazwa wakati wao walisalia eneo la ajali wakiendelea kushirikiana na watu wengine kujaribu kuvuta ndege ili kuokoa watu 19 waliosalia ndani.
Kijana Majaliwa tayari amezawadiwa fedha taslimu na ajira katika Jeshi la Zimamoto na Uokozi kwa kutambua mchango wake wa kufanikisha kuokolewa kwa abiria katika ajali hiyo.
Watu 19 akiwemo rubani Buruhani Rubaga na msaidizi wake Peter Omondi na abiria 17 walipoteza maisha katika ajali hiyo baada ya ndege kutua ndani ya maji ya Ziwa Victoria kwa kushindwa kutua uwanja wa ndege Bukoba kutokana na hali mbaya ya hewa.