Raia wa Botwasana jela miaka mitatu kuishi Tanzania kinyemela

Muktasari:

  • Theo Leborang, raia wa Botswana, amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh1 milioni na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa kosa la kuishi nchini Tanzania kinyume cha sheria.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemuhukumu raia wa Botswana, Theo Leborang kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kuishi nchini kinyume cha sheria na kutoa taarifa za uongo kwa Maofisa wa Uhamiaji.

 Hukumu hiyo imetolewa jana Jumanne Januari 11, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Francis Mhina baada ya kukiri kosa linalomkabili.

Hakimu Mhina alisema mshtakiwa alikiri kosa lake hivyo Mahakama hiyo inamtia hatiani kwa shitaka linalomkabili.

Mhina alisema kwa kuwa mshtakiwa amekiri kosa lake hivyo Mahakama hiyo inamuhukumu kulipia faini ya Sh 1 milioni au kwenda jela kifungo cha miaka mitatu.

Awali, akisoma hoja za awali Wakili wa Serikali, Hadija Masoud alieleza Januari 6, 2023 mshtakiwa huyo akiwa raia wa Bostwana alikamatwa katika eneo la Posta one stop akiishi nchini bila ya kuwa na kibali cha kuishi nchini

 Hadija alidai mshtakiwa huyo anamiliki hati ya kusafiria yenye namba BN0258427 iliyotolewa nchini Botswana ambayo imekwisha muda wake.

Katika shitaka la pili, alidai Januari 6, 2023 katika eneo la Posta one stop, Theo alitoa taarifa za uongo kuhusu utaifa wake kwa nia ya kujipatia kitambulisho cha utaifa kwa kujaza fomu namba 111011401202301050026 huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Alidai Theo alikamatwa na kufanyiwa mahojiano na alikiri alitoa taarifa za uongo yeya siyo raia wa Tanzania ni raia wa Botswana.
Hadija baada ya kumsomea maelezo ya awali aliiomba Mahakama hiyo itoe adhabu Kali ili owe fundisho kwa wengine.

"Hatuna kumbukumbu yeyote ya mshtakiwa kutenda makosa na ninaiomba mahakama hili itoe hukumu kwa mujibu wa sheria,"alidai Hadija

Akitoa utetezi wake mahakamani hapo, Theo aliiomba mahakama hiyo imsamehe kwa kuwa alidanganywa afanye hivyo itamsaidia yeye kupata uhalali wa kuendelea kuishi nchini bila kwenda katika ofisi za uhamiaji.