Raia wa Congo kortini kwa kuishi nchini kinyemela

Muktasari:

  • Raia wa Congo DRC, Mathieu Nubea amefikishwa mahakamani akikabiliwa na kesi ya kutoa taarifa za uongo na kujipatia kibali cha kuishi nchini.

Dar es Salaam. Mashahidi nane na vielelezo vinne vinatarajiwa kutolewa mahakamani katika kesi ya kutoa taarifa za uongo na kisha kujipatia kibali cha kuishi Tanzania, inayomkabili raia wa Congo DRC, Mathieu Nubea maarufu kama Emmanuel Bukasa.

Bukasa anakabiliwa kesi hiyo ya jinai namba 105/2023 iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu.

Wakili wa Serikali, Shija Sitta, ameieleza Mahakama hiyo, leo Julai 17, 2023, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mary Mrio.

Wakili Sitta amedai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya mshtakiwa kubadilishiwa hati ya mashtaka baada ya kugundulika kuwa alishawahi kushtakiwa katika kesi nyingine kwa kutumia majina mengine ambayo ni Emmanuel Kalenda Bukasa wakati huo akiwa anaishi mkoani Mbeya.

“Mshtakiwa huyu akiwa mkoani Mbeya alifunguliwa kesi ya kuishi nchini bila kuwa na kibali na hivyo alitiwa hatiani na kuamriwa na Mahakama kurudishwa nchini kwao Congo DRC," amedai Shija.

Amedai baada ya kuamriwa kurudi nchini wako, mshtakiwa huyo alirudi tena Tanzania na kujibadilisha jina, badala ya Bukasa na kujiita Mathieu Kabwe Nubea.

Akimsomea upya shtaka lake, amedai kuwa, Nubea anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 14, 2023 jiji Dar es Salaam.

Anadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa wakati akiwa raia wa Congo, na mwenye hati ya kusafiria namba OP 1221454 iliyotolewa Kinshasa Desemba 14, 2022, alitengeneza taarifa za uongo na kisha kujipatia kibali cha kuishi nchini Tanzania, kinyume cha sheria.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo, alikana kutenda kosa hilo.

Upande wa mashtaka umedai kuwa wanatarajia kuwa mashahidi nane na vielelezo vinne.

Hata hivyo mshtakiwa huyo aliomba apewe dhamana kwa kuwa shtaka linalomkabili lina dhaminika kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Mrio alimtaka mshtakiwa kuwa mdhamini mmoja anayetambulika kisheria mwenye barua kutoka Serikali ya mitaa, atakaesaini bondi ya Sh2 milioni.

Mshtakiwa ameshindwa kutumiza masharti ya dhamana na hivyo kurudishwa rumande.

Hakimu Mrio baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka ameahirisha kesi hiyo Agosti Mosi, 2023 itaanza kusikilizwa.