Rais Kabila alivyoanza kupoteza mwelekeo(4)
Muktasari:
- Tatizo la wakimbizi wa Rwanda nchini Congo liliitia doa Serikali ya Laurent Kabila tangu mwanzoni mwa utawala wake. Tatizo hilo lilitumiwa sana na wapinzani wake kuutia fedheha uongozi wake.
Tatizo la wakimbizi wa Rwanda nchini Congo liliitia doa Serikali ya Laurent Kabila tangu mwanzoni mwa utawala wake. Tatizo hilo lilitumiwa sana na wapinzani wake kuutia fedheha uongozi wake.
Hali hii ilichochewa zaidi na kitendo cha Kabila kukataa kutekeleza mageuzi ya kidemokrasia, licha ya shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Machi 22, 1997 akiwa Kisangani, Laurent Kabila alitangaza kwamba vyama vyote vya siasa vimepigwa marufuku hadi hapo “vita ya ukombozi” itakapokuwa imemalizika na kwamba “serikali ya mpito” ingekaa madarakani kwa mwaka mmoja. Hiyo ilikuwa ni Serikali ya Muungano wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Ukombozi wa Congo-Zaire (ADFL).
Katika kuidhibiti hali ya mambo, ADFL iliwapa vyeo wale tu ambao hawakuwa na uhusiano na Serikali iliyoondolewa madarakani ya Mobutu Sese Seko.
Mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yalikuwa yanajishughulisha na mabadiliko ya kidemokrasia yalipambana na ADFL wakati Kabila alipoamua kusimamisha mchakato wa demokrasia.
Waziri wa Ujenzi wa DRC, Etienne Richard Mbaya aliunda tume ya kitaifa kuratibu vitendo vya mashirika hayo ili kuyadhibiti vema.
Kwa ujumla, Kabila alitaka kupunguza nguvu ya upinzani wa ndani dhidi yake, akiutuhumu kumkubali Mobutu. Mmoja wa wapinzani hao ni Etienne Tshisekedi, ambaye kwa wakati huo alikuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha UDPS (Umoja wa Demokrasia na Maendeleo ya Jamii).
Baadaye, Kabila alitangaza kuongeza muda wa marufuku ya shughuli za vyama vya upinzani kutoka mwaka mmoja hadi miaka miwili kwa madai kwamba hakuwezi kuwa na upinzani kwa Muungano kwa sababu ADFL haikuwa chama, bali ni vuguvugu la kisiasa linalowahusu Wacongo wote.
Ingawa serikali hiyo mpya ilitangaza kwamba ingeheshimu uhuru wa kujieleza na kuruhusu vyombo vya habari kuikosoa mamlaka waziwazi, waziri wake wa mambo ya ndani, Mwenze Kongolo alitangaza kuwa maandamano yoyote na mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani ni haramu.
Magazeti kadhaa hayakusita kushutumu ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu, lakini baadaye yakagundua kuwa kile kilichoitwa ‘uhuru wa kujieleza’ kilikuwa na mipaka yake.
Wakosoaji wakali zaidi walikamatwa; kwa mfano, mwanahabari Baudoin Kamanda wa kituo cha runinga cha RTNC (Televisheni ya Taifa) alikamatwa na polisi kwa kuhudhuria mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na kiongozi wa upinzani, Arthur Z’Ahidi Ngoma.
Muda mfupi baadaye serikali ya Kabila iliigeuza RTNC kuwa chombo chake cha propaganda. Upinzani wa zamani wenye itikadi kali uliendelea kuandamana, wakitaka kuwepo kwa uhuru wa kisiasa, lakini maandamano haya yalitawanywa kwa nguvu. Ijumaa ya Julai 25, 1997, wanajeshi walifyatua risasi kwenye maandamano yaliyoandaliwa na vijana wa vyama vya PALU na UDPS, na kuua angalau mtu mmoja. Ijumaa ya Agosti 15, 1997, waandamanaji wa UDPS walikamatwa na kuteswa.
UDPS iliipinga ADFL na kujaribu kurejesha taasisi zilizowekwa na Mkutano Mkuu wa Kitaifa (CNS), ambao ulikuwa ni chombo cha kidemokrasia kilichoanzishwa chini ya Mobutu na kupendekeza kwamba zitumike kama msingi wa serikali mpya ya umoja wa kitaifa.
Ni katika hali hii ambapo Etienne Tshisekedi na Joseph Olenghankoy walikamatwa kwa muda mfupi na kuachiwa baadaye.
Maandamano ya PALU pia yalisambaratishwa kikatili, na nyumba ya kiongozi wao, Antoine Gizenga ambayo pia ilikuwa ni makao makuu ya chama, ilitekwa.
Viongozi muhimu hawakujumuishwa katika serikali ya Kabila. Mahusiano ya Kabila na familia ya Lumumba yalikuwa magumu sana, licha ya kujumuishwa kwa Juliana Lumumba (binti wa Lumumba) katika Serikali ya ADFL.
Wakati Kabila alipopanga maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 37 ya kifo cha Patrice Lumumba huko Palais du Peuple, hakuna mwanafamilia wa Lumumba aliyehudhuria sherehe hizo.
Mapema mwaka wa 1998 shirika la haki za binadamu lilichapisha orodha ya wafungwa wa kisiasa na kuweka picha zao. Miongoni mwao alikuwemo mwanaharakati wa upinzani, Mchungaji Theodore Ngoy. Wengine walikuwa waandishi wa habari kama Modeste Mutinga.
Olenghankoy na Tshisekedi walikamatwa Kinshasa Alhamisi ya Februari 12, 1998. Tshisekedi aliwekwa katika kizuizi cha nyumbani katika kijiji chake katika jimbo la Kasai. Baada ya kukamatwa, Olenghankoy alihamishiwa katika gereza la Bulowo huko Katanga.
Walipotoroka Jumapili ya Aprili 12, 1998, walikamatwa tena na kuhukumiwa vifungo gerezani. Mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia yalisema yako tayari kuisaidia DRC chini ya Kabila, lakini sharti lao kuu ni kumtaka aruhusu “utawala bora”.
Kimataifa, uadui dhidi ya Kabila ulionyeshwa wazi hata kupitia njia za kidiplomasia. Serikali ya Ubelgiji ilikuwa na mtazamo hasi kwa Kabila baada ya kunyakua madaraka Mei 1997.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Erik Derycke alitaja ukosefu wa utulivu, mshikamano wa kisiasa, na kuzuka kwa msukosuko mkubwa wa kitaifa kama sababu zilizoizuia serikali ya Ubelgiji kuendeleza uhusiano baina ya nchi hizo mbili na DRC.
Ubelgiji iliishutumu ADFL kwa kuendeleza mauaji ya kimbari upande wa mashariki. Kwa upande wake, mnadhimu mkuu wa DRC alijitokeza kwenye televisheni ya serikali na kuishutumu Ubelgiji kuwa “nchi ya kigaidi.”
Shutuma hii ilitokana na madai ya kugunduliwa kwa silaha katika ubalozi mdogo wa Ubelgiji mjini Lubumbashi. Madai haya yalikanushwa vikali na Ofisi ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji.
Licha ya juhudi fulani za wanasiasa wanaozungumza lugha ya Kifaransa kujihusisha tena na Ubelgiji nchini DRC, uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulizidi kuwa mbaya. Mtazamo huu hasi wa Kabila ulipanda mbegu ya uasi kwa siku zijazo, wakati mapambano ya kuwania madaraka kati ya makabila ya Lubakat na Watutsi yalitoa udongo wenye rutuba kwa mbegu hizo kukua.
Je, mambo yalianzaje hadi kuwa uasi kamili?
Tukutane toleo lijalo.