Rais Mahakama EAC ataja Kiswahili msingi wa haki, utawala bora
Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Jaji Nestor Kayobera.
Bujumbura. Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Jaji Nestor Kayobera amesema taasisi hiyo inatambua kuwa lugha ni msingi wa upatikanaji wa haki na utawala wa sheria, akibainisha kuwa teknolojia zinaweza kusaidia kuboresha tafsiri za nyaraka za kisheria, kuongeza upatikanaji wa taarifa za mahakama na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema maendeleo ya teknolojia za akili unde yanapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya lugha za Kiafrika, akisisitiza kuwa Kiswahili kinapaswa kuwa sehemu ya mapinduzi hayo ya kidijitali.
Akizungumza Julai 5, 2026 katika ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC) mjini Bujumbura, Burundi, Jaji Kayobera amesema kaulimbiu ya kongamano, "Kiswahili, Uwingi wa Lugha na Akili unde" inakumbusha umuhimu wa kuhakikisha maendeleo ya teknolojia hayaachi nyuma lugha za Kiafrika.
Amesema Kiswahili, ambacho ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na mojawapo ya lugha zinazokua kwa kasi duniani, kinapaswa kujumuishwa katika mifumo ya AI ili teknolojia hizo ziwe jumuishi, zenye usawa na zinazoheshimu utofauti wa lugha na tamaduni za Afrika Mashariki.
Jaji Kayobera ameeleza kuwa uwingi wa lugha ni utajiri mkubwa wa Afrika Mashariki na kwamba Kiswahili kimeendelea kuwa daraja la kuwaunganisha watu wenye lugha, tamaduni na historia tofauti katika ukanda huo.
Hata hivyo, amesisitiza matumizi ya AI yanapaswa kuzingatia uwajibikaji, uwazi, maadili na ulinzi wa haki za binadamu.
Aidha, amempongeza Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kwa kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, akisema katika kipindi hicho imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ameongeza kuwa anaamini Mpango Mkakati wa Pili wa kamisheni utaendelea kuimarisha nafasi ya Kiswahili katika elimu, utafiti, teknolojia na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Jaji Kayobera pia amewapongeza watafiti, wasomi, wabunifu wa teknolojia na vijana wanaoshiriki kongamano hilo, akisema tafiti na ubunifu wao utachangia kuandaa sera, kuendeleza teknolojia za lugha na kuifanya Afrika Mashariki kuwa mshiriki hai katika maendeleo ya akili unde duniani.
Amesema ana matumaini kongamano hilo litazaa mapendekezo yatakayochochea maendeleo ya Kiswahili, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuweka msingi imara wa matumizi ya teknolojia katika kuhifadhi na kukuza lugha za Kiafrika.