Rais mteule Kenya kutangazwa muda mfupi ujao

Muktasari:

  • Zikiwa zimesalia saa 24 kabla ya kumalizika kwa siku saba za kikatiba ilizopewa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza mshindi wa kura za urais, mwonekano wa ukumbi wa Bomas unaotumika kuhakiki na kutangaza matokeo umebadilika na inatarajiwa muda wowote kuanzia sasa mshindi anaweza kutangazwa.

Nairobi. Zikiwa zimesalia saa 24 kabla ya kumalizika kwa siku saba za kikatiba ilizopewa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza mshindi wa kura za urais, mwonekano wa ukumbi wa Bomas unaotumika kuhakiki na kutangaza matokeo umebadilika na inatarajiwa muda wowote kuanzia sasa mshindi anaweza kutangazwa.

Mpaka jana matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 yaliyokuwa yakitangazwa na vyombo vya habari yalionyesha kuwa mgombea wa Kenya Kwanza William Ruto alikuwa akiongoza kwa kupata kura milioni 6.7 na mgombea wa Azimio la Umoja, Raila Odinga alikuwa na kura milioni 6.6.

Tayari watu mbalimbali ikiwemo waandishi wa habari wameshaketi kwenye ukumbi huo wakiwasubiri maofisa IEBC, kutoa taarifa walizonazo juu ya matokeo ya urais.

Awali ukumbi huo kwenye eneo la katikati ambalo lilikuwa linatumika kwenye kuhesabia kura (auditorium) lilikuwa na meza nane huku zikiwa zimepangwa kwa mfumo wa duara lakini asubuhi ya leo, Jumatatu Agosti 15, 2022 meza hizo zimeondolewa na zilizopo zimepangwa kwa muundo wa watu kutaka kuhutubia na sio kuhakiki kura tena.

Pia, kwenye upande ambao wanadiplomasia wakiwemo wasimamizi wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi eneo hilo lilikuwa na idadi ndogo ya watu lakini leo idadi imekuwa maradufu.

Kwaya mbalimbali zimepewa fursa ya kutumbuiza hali ambayo ni tofauti na siku sita zilizopita tangu, uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 ulivyofanyika.

Ishara hii inasemwa huenda muda wowote kuanzia sasa, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati atatamgaza matokeo ya urais nchini.