Rais Museveni awasili Tanzania kwa ziara ya siku tatu

Saturday November 27 2021
musevenipic
By Sharon Sauwa

Dodoma. Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni amewasili nchini leo Jumamosi Novemba 27, 2021 kwa ziara ya siku tatu ambapo amepokelewa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Baada ya kupokelewa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Rais Museveni na mwenyeji wake wamekagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21.

Baada ya kukamilisha mapokezi hayo taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano Ikulu jana Novemba 26, 2021  ilisema marais hao wataelekea Ikulu ya Dar es Salaam kwa mazungumzo ya faragha.

Rais Museveni na mwenyeji wake Rais Samia watashiriki katika ufunguzi wa kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uganda ambalo pamoja na masuala mengine litajikita katika sekta ya mafuta na gesi.

Aidha, atatembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukagua mradi unaoendelea wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Stesheni Kuu.

Advertisement

Pia, Museveni atakwenda Wilayani Chato, mkoani Geita ambapo ataikabidhi rasmi Serikali ya Tanzania shule ya msingi iliyojengwa kwa ufadhili wake Wilayani humo na baadaye kuitembelea familia ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Magufuli.

Mara baada ya shughuli hizo, Rais Museveni atahitimisha ziara yake ya siku tatu nchini na kuagana na mwenyeji wake Samia.


Advertisement