Rais Mwinyi akitaka Chuo cha Mafunzo zanzibar kujifunza Magereza

Muktasari:

  • Rais Mwinyi amezindua miradi minne ya maendeleo katika Gereza la Mkono wa Mara mkoani Morogoro, huku akitaka Chuo cha Mafunzo Zanzibar kuchota uzoefu wa kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka kwa Jeshi la Mazingira.

Morogoro. Rais wa Zanzabar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amezindua miradi minne ya maendeleo katika Gereza la Mkono wa Mara, huku akitaka Chuo cha Mafunzo Zanzibar kuchota uzoefu wa kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka kwa Jeshi la Magereza.

Dk Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 15, wakati akizindua miradi kiwanda cha maziwa, ujenzi ngome ya gereza hilo, ujenzi kituo cha huduma cha Mama na Mtoto na ujenzi wa nyumba za maofisa na askari wa Jeshi la Magereza.

Akizungumza na wananchi kwenye hafla ya uzinduzi huo mkoani Morogoro, Rais Dk Mwinyi amesema Chuo cha Mafunzo Zanzibar kina kila sababu ya kufika Bara kujifunza namna miradi mbalimbali inavyotekelezwa na Jeshi la Magereza Tanzania.

Mbali na Chuo cha Mafunzo Zanzibar, pia amezitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa jeshi hilo ili miradi inayotekelezwa iwe chachu ya kujikwamua kiuchumi.

“Kiwanda hiki kitanufaisha watu wengi na sasa ijiitangaze kwa jamii ili kupata malighafi za kuzalisha zaidi maziwa kwani miradi hii inavyotekelezwa ni dhahiri italeta manufaa. Viongozi wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar waje kuja kujifunza miradi inayotekelezwa na hawa Magereza,” amesema Dk Mwinyi.

Kwa upande wake Waziri wa wizara ya Mambo ya Ndani, George Simbachene amesema kuwa Jeshi la Magereza kwa sasa lina uwezo wa kulisha wafungwa kwa asilimia 100 na hivyo limeokoa takribani Sh1 bilioni kwa mwezi kulisha wafungwa na mahabusu.

“Kila kambi wanatekeleza miradi ya nyumba na tummekalisha zaidi ya nyumba 400 ili kuhakikisha askari wetu na maafisa wetu wanaishi katika makazi bora,” amesema Waziri Simbachewene.

Naye Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Seleman Mzee, amesema kuwa jeshi la magereza limejikita katika mabadiliko kwa kutakiwa kujitegemea katika uendeshaji wake na kujitegemea katika ujenzi wa nyumba za askari na maofisa wake.

Kamishna Mzee alisema kuwa hatua ya kuzindua miradi minne Morogoro ni moja ya miradi mingine ambayo imefikia hatua ya kuwekewa mawe ya msingi nchi mzima.