Rais Mwinyi aridhia Simai kujiuzulu, CCM wampongeza

Muktasari:
- Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Januari 26, 2024 ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said imeeleza kuwa Dk Mwinyi amekubali ombi hilo la kujiuzulu.
Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi ameridhia ombi la Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Muhammed Said kujiuzulu nafasi yake.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Januari 26, 2024 ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said imeeleza kuwa Dk Mwinyi amekubali ombi hilo la kujiuzulu.
“Kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini kifungu 129 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amekubali ombi la kujiuzulu, Simai Mohamed Said, Waziri wa Mambo ya Kale kuazia Januari 26, 2024,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Awali katika taarifa yake ya kujiuzulu iliyokuwa katika mfumo wa picha jongefu kisha ikathibitishwa na Charles Hilary, Msemaji wa Serikali ya Mapinduzi, Simai alisema amefikia uamuzi huo ambao sio rahisi katika utamaduni wa Zanzibar, lakini kutokana na imani yake kwamba jukumu la wasaidizi wa Rais, wakiwemo mawaziri ni kumsaidia katika kutekeleza ilani ya chama (CCM.
Wakati huo huo Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho Simai ni mwanachama wake akihudumu kwenye Jimbo la Tunguu Visiwani humo, kimesema kuwa kujiuzulu ni jambo la kawaida na kiongozi huyo ameonyesha mfano bora.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 26, 2024 Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbeto amesema kujiuzulu ni jambo la kawaida na Simai ameonyesha mfano bora.
“Hatuna shida nayer, kujiuzulu ni jambo la kawaida na kwangu naona ameonyesha mfano bora,”amesema Mbeto.