Waziri wa Utalii Zanzibar ajiuzulu

Muktasari:

  • Kupitia video iliyosambaa mitandaoni amesema mazingira ya kazi si rafiki, hivyo ameamua kujiuzulu.

Ugunja. Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Simai Mohamed Said, ametangaza kujiuzulu wadhifa huo.

Kupitia video iliyosambaa mitandaoni usiku wa kuamkia leo Januari 26, 2024 Simai amesema amejiuzulu kutokana na alichodai mazingira yasiyo rafiki ya kazi.

Simai pia ni mwakilishi wa Tunguu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na Msemaji wa Serikali, Charles Hilary amethibitisha kujiuzuli kwa waziri huyo.

Katika taarifa aliyorekodi kwenye picha jongefu (video), Simai amesema:

"Nimeandika barua ya kujiuzulu nafasi yangu kuanzia leo (jana Januari 25,2024) Nimefikia uamuzi huu ambao si rahisi katika utamaduni wetu.”

“Kutokana na hilo jukumu namba moja la wasaidizi wa Rais ni kumsaidia kutekeleza ilani na inapotokea mazingira yasiyo rafiki katika kutekeleza jukumu hilo la ustawi wa wananchi, ni vyema kutafuta jawabu kwa haraka ili kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo iweze kuendelea hata ikibidi kukaa pembeni," amesema.

Amesema amefikia uamuzi huo mgumu wa kukaa pembeni.