Rais Mwinyi atoa pole kwa familia kifo cha Raza

Rasi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi

Muktasari:

  • Rasi wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ametoa salamu za pole kwa familia jamaa na ndugu kufuatia kifo cha mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu visiwani Zanzibar, Mohmed Raza.

Unguja. Rasi wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ametoa salamu za pole kwa familia jamaa na ndugu kufuatia kifo cha mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu visiwani Zanzibar, Mohmed Raza.

Raza amefarikid dunia leo Juni 8, 2023 katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.

Katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo Juni 8, 2023 Rais Mwinyi ameisihi familia ya marehemu kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo

“Namuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu pema peponi,”

Taarifa za kifo hicho zimethibitishwa leo Juni 8, 2023 na mwanafamilia Mohamed Ibrahim (Raza Lee) amesema msiba upo Aga Khan na mazishi yatafanyika saa 11:00 jioni katika makaburi ya Kisutu.

Wakati huo huo Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kimepokea kwa masikitiko kufuatia kifo hicho mwanasiasa huyo

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kamati Malumu, Itikadi na Uenezi, CCM Zanzibar, Khamis Mbeto amesema chama kimeondokewa na mtu mchapakazi na mpenda haki.

“Enzi za uhai wake Mohamed Raza alikuwa ni kiongozi aliyelinda na kukipigania chama chetu na alikuwa ni kada muadilifu, mchapakazi na mzalendo mwenye maono ya kimaendeleo ndani ya chama na Serikalini”,

Raza alizaliwa Julai 8, 1962 Mtaa wa Mkunazini Unguja, hadi anafariki alikuwa ni kada wa CCM. Amewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali ndani ya CCM akiwa mwakilishi wa Uzini na Serikali aliwahi kuwa mshauri wa Rais wa Zanzibar Awamu ya Tano katika masuala ya michezo.

Ameugua kwa kipindi kirefu na kulazwa hospitalini ambapo kwa nyakati tofauti viongozi wakuu wa kitaifa, Rais Mwinyi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud walimtembelea na kumjulia hali.