Rais Mwinyi awataka wauguzi kutumia lugha nzuri

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka wauguzi wote kuwa na moyo wa huruma, kutumia lugha nzuri na kufuata maadili ya taaluma yao wakati wote wanapotoa huduma kwa wagonjwa.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 12, 2023 wakati wa kilele cha siku ya wauguzi duniani kisiwani humo ambapo amesema bila ya wauguzi kutekeleza vyema majukumu yao, afya ya jamii na maisha yao kwa jumla yanakuwa mashakani.

“Lazima muwe na moyo wa huruma mtoe huduma bora kwa kuzingatia misingi na weledi wa taaluma yenu, hapana shaka kwamba, bila ya wauguzi kutekeleza vyema majukumu yao, afya ya jamii na maisha yao kwa jumla yako mashakani,” amesema Dk Mwinyi. 

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema wauguzi wetu ni mustakabali wetu, Dk Mwinyi alisema imechaguliwa ili kuonesha nafasi muhimu ya mchango unaotolewa na wauguzi katika kuleta ustawi wa maisha katika jamii duniani kote.

Hata hivyo amewapongeza baadhi ya wauguzi ambao wanafanya kazi vizuri kwa uadilifu na kujituma usiku na mchana bila ya kuchoka ya kuhudumia wagonjwa na kuwasihi kuendelea na kuwa na moyo huo ili kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Akisoma risala kwa niaba ya wauguzi wenzake, muunguzi Said Kheir Hamad, amesema wauguzi wametoa mchango mkubwa duniani kupunguza vifo vya watoto wachanga, malaria, Ukimwi na maradhi mengine.

Hata hivyo amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uchache wa wauguzi kulingana na wagonjwa wanaowahudumia.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya za Wauguzi Zanzibar (Zana), Dk Rukia Rajab amesema pamoja na kada hiyo kukabiliwa na changamoto nyingi, zisiwakatishe tamaa bali wazibadilishe kuwa fursa.