Rais Samia aahidi kuwapa kazi makandarasi wa ndani

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amewapigia simu wahandisi na makandarasi waliokuwa na kongamano la kumpongeza na kuahidi kuwapa miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali.

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassani amesema Serikali itakuwa karibu na wahandisi kwa kuwapatia miradi midogo na mikubwa inayokuja kuwapatia ili kuendelea kuiheshimisha nchi.

Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 4, 2022 kwa simu baada ya kuona kongamano la wahandisi na makandarasi lililokuwa na lengo kumpongeza ililofanyika jijini hapa

“Nawaahidi Serikali itakuwa karibu na wahandisi na kuhakikisha katika miradi midogo na mikubwa inayokuja mtapata nafasi nyingi ya kufanya kazi kama makandarasi wazawa hii itatupa heshima ya kuendelea kuitangaza nchi yetu.

“Niseme tu mjipange vizuri kufanya kazi kuna miradi mikubwa inakuja hivi karibuni nitahakikisha mnapata nafasi ya kuifanya,” amesema Rais Samia.

Awali akizungumza na makandarasi na wahandisi wa miundombinu Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya aliyekuwepo katika kongamano holo, amesema Serikali itahakikisha inawajengea uwezo wakandarasi wazawa ili kuhakikisha wanapata fursa ya miradi mikubwa hapa nchini.

Pia, amewataka kufanya kazi kwa uzalendo na ufanisi kama Watanzania na kuacha ubadhilifu kwenye utekelezaji wa miradi.

Amesema kuwa uchumi wa Tanzania unaitegemea sekta ya ujenzi na uchukuzi ndio maana Rais Samia alistahili tuzo hiyo kutokana na kutekeleza nguvu katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo bababara, reli, bandari na hata viwanja vya ndege

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amewashukuru wakandarasi na wahandisi kwa kufanyia kongamano lao mkoani humo.

Mtaka amewataka makandarasi hao kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa weledi.

“Tubebe matamanio ya kufanya kazi kwenye miradi mikubwa hata ya nje ya nchi. Kuna makandarasi wengi wa nje wapo nchini na sasa muone namna kutoka nje nchi na kutafuta kazi za ukandarasi,” amesema Mtaka.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakandarasi Wazalendo Tanzania, Thobias Kyando amesema kuwa serikali imekuwa ikitekeleza miradi mingi ya ujenzi huku wakandarasi wazawa wakiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema kulingana na takwimu zilizopo, kati ya miradi ya Sh4.9 trilioni, wakandarasi wa ndani walipata kazi za Sh 2.9 trioni, huku wakandarasi wa nje wakipata Sh2.1 trilioni, jambo alilosema Serikali imeonesha kuwathamini wakandarasi wa ndani.