Rais Samia aahidi ushirikiano na Marekani

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris ambapo, pamoja na mambo mengine wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris ambapo, pamoja na mambo mengine wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo.

Pia, wawili hao wamejadili masuala mbalimbali katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii ambapo, Rais Samia amesisitiza kuendelea kujenga mazingira bora ya kiuchumi na kisiasa.

Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Aprili 15, 2022, viongozi hao walikuwa na mazungumzo ya faragha jijini Washington, Marekani.

Katika mazungumzo yake, Rais Samia ameishukuru Marekani kwa ushirikiano na misaada yake inayopitia katika Shirika la Misaada la nchi hiyo (USAID), zikiwemo chanjo za Uviko-19. 

“Tanzania tunashukuru kwa msaada wa chanjo za Uviko-19 mlizotusaidia kupitia mpango wa Covax. Ninyi pekee mmetupatia dozi karibu milioni tano ambazo zimekuwa na msaada mkubwa kwetu,” amesema Rais Samia.

Pia, Rais Samia amezungumzia haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia nchini ambapo, amesema Tanzania imeweka mikakati madhubuti katika maeneo hayo.

Amesema Tanzania imechukua hatua za makusudi kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania. “Tunajitahidi kuchukua hatua za makusudi ili kuona kunakuwa na ushirikishwaji, umoja na mshikamano miongoni mwa vyama na Watanzania kwa ujumla,” amesema.

Kuhusu vyama vya siasa, Rais Samia amesema kumekuwa na mikutano ya wadau ikiwa ni jitihada za makusudi kutafuta njia sahihi za kuendesha siasa safi kwa kulinda maslahi ya Taifa.

Katika eneo la biashara na uwekezaji, Rais Samia amesema Tanzania inaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi ya kufanyia biashara na tayari Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeweka mazingira rafiki katika kutekeleza hayo.

“Ombi langu kwa Serikali ya Marekani ni kuhamasisha zaidi sekta binafsi ya nchini hapa kuja kufanya kazi na Tanzania, tuna fursa nyingi hivyo karibuni,” amesema na kuongeza: Sekta binafsi Tanzania ipo katika hatua ya kutengeneza sheria ya uwekezaji ambayo itatengeneza mazingira bora zaidi kwa wawekezaji.

Kwa upande wake, Kamala amesema mazungumzo hayo yamelenga kuinua uchumi wa Tanzania hasa kwa kuangalia fursa za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo utalii.

Amesema eneo lingine ambalo wamezungumza na mgeni wake (Rais Samia) ni kuhusu sekta ya afya likiwemo janga la Uviko- 19 na kukubaliana kushirikiana.

Rais Samia yuko nchini Marekani kuhudhuria uzinduzi wa filamu ya Royal Tour ambayo imetengenezwa mahususi kutangaza fursa za uwekezaji na utalii.

“Uamuzi wa kuichagua Marekani kwa ajili ya uzinduzi haukuja kwa bahati mbaya, tumefanya  kwa makusudi tukifahamu kuwa ndipo walipo wanaopenda kufurahi,” amesema.