Rais Samia afunga na mambo sita
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amehitimisha siku 150 za mbio za Mwenge wa Uhuru zilizoenda sambamba na maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere huku akiweka kipaumbele katika mambo sita.
Chato/Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan amehitimisha siku 150 za mbio za Mwenge wa Uhuru zilizoenda sambamba na maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere huku akiweka kipaumbele katika mambo sita.
Vipaumbele hivyo alivyovitoa katika hafla ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye Uwanja wa Magufuli mjini Chato jana ni usimamizi na umakini katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kumuenzi mtangulizi wake hayati John Magufuli kwa kukamilisha ahadi na miradi aliyoianzisha, kujikinga na maradhi pamoja na matumizi ya Tehama.
“Kwa kawaida sherehe za Mwenge wa Uhuru hufanyika kwenye makao makuu ya mkoa, Chato imepata nafasi ya kipekee kuwa mwenyeji wa sherehe za mwaka huu kama sehemu ya kumuenzi mpendwa wetu hayati John Magufuli. Nataka niwahakikishie kwamba Serikali itatekeleza miradi yote ya maendeleo aliyoiasisi,” alisema Rais Samia.
Huku akishangiliwa na umati uliohudhuria hafla hiyo iliyowakusanya viongozi wakuu wa kitaifa, Rais Samia alitaja baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Chato ni ujenzi wa uwanja wa ndege, Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), stendi ya mabasi na msikiti unaojengwa katika Kijiji cha Muungano.
Katika hotuba yake ya zaidi ya dakika 40, kiongozi huyo mkuu wa nchi alisema Serikali inakamilisha vigezo vitakavyowezesha kukamilika kwa mchakato wa kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato.
“Serikali inakamilisha vigezo vinavyoruhusu Chato kuwa mkoa, haujawa bado mkoa; kuna vigezo kadhaa tunavyoendelea kuviangalia. Vigezo hivyo vikikidhi, tunakwenda kulimaliza jambo hili (la Chato kuwa mkoa),” alisema Rais Samia akizungumzia mchakato unaoendelea wa kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato.
Ma-RC, DC na DED mtegoni
Akizungumzia taarifa ya miradi 49 ya maendeleo yenye thamani ya Sh65.3 bilioni iliyokataliwa na kiongozi wa mbio ya Mwenge wa Uhuru 2021, Luteni Josephine Mwambashi kwa kutiliwa shaka ubora kulinganisha na thamani halisi ya fedha, Rais Samia aliwaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuongeza umakini katika utekelezaji na usimamizi wa miradi katika maeneo yao.
“Nimeelezwa miradi 49 yenye thamani ya Sh65.3 bilioni imekataliwa na Mwenge kwa kutiliwa shaka, kuhusu ubora na thamani ya fedha; viongozi wa maeneo husika wanakuwa wapi wakati miradi inatekelezwa chini ya kiwango? Hii ni ishara kuwa hakuna ufuatiliaji,” alisema Rais Samia.
“Idadi ya miradi yenye dosari ipungue wakati mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022. Hii iwe ni onyo kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.”
Awali, akitoa taarifa ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema miradi 49 yenye thamani ya Sh65.3 bilioni ilikataliwa katika wilaya 38 kati ya 150 zilizotembelewa na mwenge.
Waziri Mhagama alisema tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeanza kuchunguza miradi hiyo na taarifa itawasilishwa kwa Rais kwa uamuzi, maelekezo na hatua zaidi.
Mwenge wa Uhuru umekimbizwa umbali wa kilometa 21,480. 16 ukipita wilaya 150 kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 1, 067 ya sekta ya afya, maji, umeme, uvuvi, kilimo, ufugaji, elimu na miundombinu yenye thamani ya zaidi ya Sh1.2 trilioni.
Chuo Kikuu cha Tehama
Kuhusu maendeleo ya teknolojia na maendeleo, Rais Samia alisema pamoja na utekelezaji wa mradi miundombinu ya mkongo wa Taifa, Serikali inakusudia kujenga Chuo Kikuu cha Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) kitakachokuwa kikubwa kuliko vyote ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, huku akiwataka vijana kutumia fursa hiyo kwa ajili ya maendeleo.
“Tumeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika vifaa vya Tehama ikiwamo simu janja, vishikwambi, modemu huku tukiendelea na tafiti za kisayansi zitakazowezesha vijana kutumia fursa zinazoambatana na maendeleo ya teknolojia.
“Serikali pia inatekeleza mikakati na miradi ya kutambua ubunifu wa vijana; lengo ikiwa ni kuwawezesha vijana wa Kitanzania si tu kuwa wabunifu kitaifa, bali pia kimataifa,” alisema Rais Samia.
Hata hivyo, aliwaasa vijana nchini kutumia vema fursa na maendeleo ya teknolojia kwa sababu ikitumika vibaya inaweza kusababisha madhara kwa jamii ikiwamo mifarakano, wizi wa kimtandao, ugaidi na hata vita.
Bangi, magonjwa ya akili na Uviko-19
Pamoja na kuwapongeza vijana kwa kushiriki katika harakati na juhudi za maendeleo, Rais Samia aliwataka kujiepusha na magonjwa yakiwamo ya akili yanayochochewa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya dawa za kulevya.
“Vijana ndiyo nguvu na injini ya maendeleo na uhai wa Taifa lolote duniani kwa sababu hili ndilo kundi kubwa la watu wenye nguvu na uthubutu; Serikali itaendelea kuwapa elimu, stadi za maisha na fursa. Nawasihi vijana wachukue tahadhari na kujilinda dhidi ya maradhi na mambo mengine yanayoweza kuathiri ustawi wao na Taifa,” alisema Rais Samia.
Alitaja maeneo mengine ambayo vijana wanapaswa kuchukua tahadhari kuwa ni maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) na Uviko-19.
Rais Samia alisema Serikali itaendelea kutimiza wajibu wa kukabiliana na kudhibiti dawa za kulevya ikiwamo tabia ya baadi ya watu wanaoendelea kulima bangi katika safu za milima na mabonde nchini.
Kuhusu Uviko-19, aliwahimiza Watanzania kila mtu kwa nafasi na eneo lake kuzingatia kanuni za afya kujikinga na kuwakinga wengine kwa kunawa mikono kwa sababu na maji tiririka, kuvaa barakoa na kuchanja.
“Afya ndiyo mtaji wa maisha na maendeleo, kila mmoja atimize wajibu wa kulinda afya yake na ya wengine. Ni muhimu kupima na kutambua afya mara kwa mara,” alisema.
Pia, aliwataka Watanzania kuendelea kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na malaria huku akisema ni tishio pamoja na maradhi mengine yasiyoambukiza kama kisukari, saratani na shinikizo la damu.
Mbio za Mwenge za kipekee
Katika taarifa yake kwa Rais Samia, Waziri Mhagama alisema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zilikuwa za kipekee kwa Watanzania kulinganisha na miaka iliyopita.
Alisema mbio za mwaka huu zimefanyika wakati Taifa likielekea kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru ifikapo Desemba 9 huku kukiwa na mabadiliko ya ghafla katika nafasi ya urais kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka huu.
“Tumekimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka huu huku Taifa likiwa limewapoteza viongozi wakuu wawili; Rais Magufuli aliyefariki akiwa madarakani na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa,” alisema Waziri Mhagama.
Dk Mwinyi ahimiza amani
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliwaasa Watanzania kuilinda amani iliyopo nchini na kuwezesha Tanzania kuendelea kuwa kitovu cha amani katika bara la Afrika na mfano wa kuigwa duniani.
Alisema hayo katika misa takatifu iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Bikira Maria mjini Chato. Misa hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaombea viongozi waliopo madarakani akiwamo Rais Samia.
Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi alisema ni jambo jema kwa viongozi wa Serikali kuwashirikisha viongozi wa dini katika shughuli na maadhimisho ya kitaifa ikiwamo kuwaombea viongozi waliotangulia mbele za haki.
Nyerere aenziwe kivitendo
Wakizungumzia jinsi ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mwanza waliwataka viongozi waliopo madarakani na Watanzania kwa jumla kumuenzi kivitendo mwasisi huyo wa Taifa kwa kuhimiza uzalendo, uongozi bora unaojali haki, utu na usawa kwa wote.
Mkazi wa Nyamagana, Abdul alisema: “Mwali Nyerere alikuwa mzalendo wa kweli, hakuwa mnafiki wala mbinafsi, alitetea Taifa na watu wake dhidi ya aina yoyote ya ubaguzi na ukandamizaji. Alichukia dhulma. Viongozi waliopo waige mfano huo, wasifumbie macho uovu wala kuwafumba midomo wanaokemea.”
Abdul alisema Mwalimu Nyerere si tu kama mtetezi wa wanyonge, bali pia alikuwa jemadari katika vita dhidi ya umaskini, maradhi na ujinga aliyotaja kama moja ya maadui wa Taifa.
Johari Shabani, mkazi wa mtaa wa Tambukareli jijini Mwanza, alisema kupitia historia na hotuba mbalimbali za Mwalimu Nyerere, amegundua kuwa mwasisi huyo wa Taifa alichukia ukabila, udini, ukanda na upendeleo wa aina yoyote.
“Alifanikiwa kuondoa ukabila nchini, hivyo nawaomba viongozi hasa wanasiasa wasitumie ukabila kuwatenganisha Watanzania kwa masilahi yao,” alisema Johari.