Rais Samia agusia yanayomkwaza kwa mawaziri

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaapisha mawaziri watatu huku akitoa angalizo kwa mambo matatu yanayoweza kumkwaza katika utekelezaji wa majukumu yao; utii katika maelekezo wanayopewa na Serikali, utunzaji wa siri za Serikali na utetezi wa katiba ya nchi bila kubagua upande.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaapisha mawaziri watatu huku akitoa angalizo kwa mambo matatu yanayoweza kumkwaza katika utekelezaji wa majukumu yao; utii katika maelekezo wanayopewa na Serikali, utunzaji wa siri za Serikali na utetezi wa katiba ya nchi bila kubagua upande.

 Rais Samia anatoa maelekezo hayo leo Oktoba 3, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa viapo vya wateule hao baada ya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kuwahamisha wawili, kumuondoa mmoja na kumrejesha Angella Kairuki bungeni kisha kumteua kuwa waziri.

Rais Samia amemuapisha Kairuki ambaye alimteua kuwa mbunge wa Bunge la Tanzania kisha kumteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) huku akimweka kando, Balozi Liberata Mulamula aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Rais Samia Suluhu Hassan, akimuapisha Angellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Oktoba 3, 2022.

Pia amemuapisha Dk Stergomena Tax aliyechukua nafasi ya Balozi Mulamula pamoja na Innocent Bashungwa aliyekuwa Waziri wa Tamisemi aliyemuhamishia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuchukua nafasi ya Dk Tax.

Katika hotuba yake, Rais Samia amewataka kuishi viapo vyao kwa kuilinda Jamuhuri ya Muungano. “Mnaposema mtaheshimu, mtailinda na kuitetea, hiyo ni Katiba ya Jamuhuri ya Muungano, Muungano wenye pande mbili na mtatumika sehemu zote sawa,”amesema Rais Samia akifafanua.

Rais Samia Suluhu Hassan akimuapisha Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Oktoba 3, 2022. Picha na Ikulu

“Jambo la pili mnatakiwa kujua mipaka, kwamba nchi hii ina mamlaka na mamlaka uliyowekewa ina ukomo wake, unapotaka kuvuka lazima upate ruhusa.”

Jambo la tatu Rais Samia amesema mawaziri hao wanatakiwa kutunza siri za pande zote za muungano. “Linaloamuliwa na serikali ni jambo lako, unatakiwa kulifanyia kazi kwa maelekezo, huwezi kusema nimeelekezwa hivi mimi sikutaka hivi, imebidi nifanyie hivi kwa sababu nimeelekezwa, huwezi kujitoa, kwa hiyo nilitaka kuwaambia hayo matatu.”

Rais Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dk Stergomena Lawrence Tax kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Oktoba 3, 2022. Picha na Ikulu

Balozi Mulamula amehudumu katika wizara hiyo kuanzia Machi 31, 2021 alipomteua kuwa Mbunge kisha kumteua kuwa waziri wa mambo ya nje kuchukua nafasi ya Profesa Palamagamba Kabudi