Kairuki aapishwa kuwa mbunge

Muktasari:

Angela Kairuki ameapishwa kuwa Mbunge na Spika Tulia Ackson muda mfupi kabla ya kuapishwa kuwa Waziri wa Tamisemi.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amemuapisha Angela Kairuki baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uapisho huo umefanyika leo Oktoba 03, 2022 saa 9:03 asubuhi katika Ofisi Ndogo za Bunge ikiwa ni saa chache tangu Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ilipotoa taarifa ya uteuzi huo.

Akizungumza baada ya kumuapisha mbunge huyo mpya, Spika Tulia amesema Bunge litampatia ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake aliyokasimiwa na Rais Samia.

"Sisi kama Bunge tunakutakia kila la heri. Wizara unayokwenda ni kubwa, ina mambo mengi. Ndiyo wizara ambayo iko karibu na wananchi, fedha nyingi zinaelekezwa huko.

"Bunge tunakuahidi ushirikiano kwako katika majukumu ambayo Rais ameyakasimu kwako," amesema Spika wakati wa hafla hiyo fupi iliyochukua dakika nane.

Kairuki ambaye ameteuliwa pia kuwa Waziri katika Ofis ya Rais - Tamisemi, ameapishwa pia na Rais Samia, hakutaka kuzungumza, badala yake aliondoka moja kwa moja kuelekea Ikulu kwa ajili ya kiapo kingine cha uwaziri.

Kairuki amekuwa mbunge wa viti maalumu na waziri katika wizara mbalimbali katika serikali za awamu ya nne na ya tano.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, hakufanikiwa kupita kwenye kura za maoni za CCM wakati akiwania kupitishwa kuwa mgombea ubunge katika jimbo la Same Magharibi.