Rais Samia amuagiza bosi mpya Tanesco asisikie kelele za kukatika umeme

Muktasari:

  • Rais Samia amtaka mkurugenzi mtendaji mpya wa Tanesco, kuhakikisha anasimamia ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme, akisema ndani ya miezi sita hataki kusikia kelele za umeme.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amempa miezi sita bosi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana nchini.

Amemtaka bosi huyo wa zamani wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kwenda kusimamia mchakato wa ukaratabati wa mitambo unaoendelea hivi sasa, akisema ndiyo kazi yake ya kwanza ndani ya Tanesco.

Rais Samia amesisitiza kuwa baada ya miezi sita hataki kusikia kelele za kukatika kwa umeme, hata hivyo, Rais Samia amesema Nyamo-Hanga anaiweza kazi hiyo na watampata ushirikiano.

“Nyamhanga una miezi sita nisisikie kelele za kukatika kwa umeme inakuaje… Maharage (Chande bosi wa zamani wa Tanesco) yupo hapo akuambie walikuwa wanafanyaje wanapenya wapi.

“Najua utaweza nakupa miezi sita, nakuangalia pale Tanesco, kazi yako ya kwanza ni kusimamia ukarabati wa mitambo, lakini baada ya miezi sita, nisisikie kelele za kukatika kwa umeme,tutasaidiana nenda najua utaweza,” amesisitiza Rais Samia.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo Jumanne Septemba 25,2023 Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni kwa nyakati tofauti.

Katika hotuba yake, Rais Samia amekiri uwepo wa changamoto ya umeme hivi sasa akisema janga hilo siyo la mtu bali ni la Taifa. Amesema hali hiyo inatokana na mabadiliko ya tabia ya nchi sambamba na mchakato wa matengenezo ya mitambo.

“Nyamo-Hanga unakwenda Tanesco nakujua kwamba wewe si mgeni, unaijua vyema utakwenda kuongeza pale Maharage alipofikia tuna ‘crisis’ (janga) kama Taifa siyo mtu. Bali mitambo haikufanyiwa matengenezzo kwa muda mrefu, sasa inakwenda kufanyiwa matengengezo.

“Inapofanyiwa matengenezo lakini kwingine kuzimwe na kuwasha kwa hiyo kuna upungufu wa umeme, lakini kuna mabadiliko ya hali ya hewa hasa jua kali na maji yamepungua …,” amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Serikali imejipanga katika kukabiliana na suala hilo, ikiwemo kufanya ukarabati wa mashine, kujenga vituo vya kupoza umeme, kuunganisha mikoa katika gridi ya Taifa.