Rais Samia aonya uharibifu wa barabara

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuacha tabia ya kuharibu miundombinu ya barabara, akisema kufanya hivyo kunasababisha hasara ya fedha zilizotumika kujenga.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuacha tabia ya kuharibu miundombinu ya barabara, akisema kufanya hivyo kunasababisha hasara ya fedha zilizotumika kujenga.

Rais Samia ametoa rai hiyo jijini Arusha leo, Ijumaa Julai 22, 2022 wakati wa hotuba yake katika ufunguzi wa barabara ya Afrika Mashariki (Arusha Bypass) yenye urefu wa kilomita 42.4.

“Niwaombe sana ndugu zangu kufuata taratibu zilizowekwa ili tuendelee kutunza miundombinu yetu, iendelee kutukuzia uchumi wetu,” amesema.

Ametaja baadhi ya tabia zinazoharibu miundombinu kuwa ni kumwaga mafuta barabarani, kuzidisha uzito wa mizigo kwenye magari, kutupa taka kwenye madaraja na kuchimba mchanga.

Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Rogatus Mativila amesema Sh197.45 bilioni zimetumika kugharamia ujenzi huo.

Amesema Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania ndizo zilizogharamia ujenzi huo uliofanyika kwa kipindi cha miezi 46.