Rais Samia apongezwa kukipaisha Kiswahili kimataifa

Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni, Dk Pindi Chana (kushoto) akimsikiliza Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita). Consolota Mushi (aliyesimama) wakati akielezea mpango kazi wa baraza hilo baada ya waziri huyo na Naibu wake Pauline Gekul kutembelea ofisi za baraza hilo Kijitonyama jijini Dar es Salaam leo Jumatano. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tafsiri na Ukalimani, Vida Mutasa.

Dar es Salaam. Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni, imepongeza juhudi zinazoonyeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni, Dk Balozi Chana ameyasema hayo leo Jumatano, Februari 22,2023 wakati wa ziara ya kuzitembelea taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, akiwa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) kwenye ofisi zake Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Dk Pindi Chana amesema miongoni mwa mambo mengi ya kupongezwa katika maendeleo na ukuaji wa Kiswahili ni pamoja na juhudi za Rais Samia jinsi ambavyo amekuwa akitumia katika majukwaa ya kimataifa.

"Hivi karibuni Rais Samia amehutubia kwa lugha ya Kiswahili katika mkutano wa kimataifa jambo ambalo linaleta hamasa zaidi," amesema.

 Ameongeza kuwa, "Tunapaswa kumshukuru na kutambua pia mchango wa Mwalimu Julius Nyerere, kutokana na msingi aliotuwekea kama Taifa kwa kutumia Kiswahili kuunganisha makabila yote nchini," alisema.

 Waziri Chana amesema nia ya serikali kuliwezesha baraza hilo ili lifanye kazi zake kwa ufanisi na kuzifikia nchi nyingi katika kukuza na kuendeleza Kiswahili ulimwenguni.

Aidha, Balozi Chana alisema ipo haja ya kuangalia upya Sheria ya Bakita ya mwaka 1967 iwapo inahitaji mabadiliko ili kuendana na mahitaji ya sasa ambapo Kiswahili kimekuwa lugha ya kimataifa.

Dk Chana ameliagiza baraza hilo kuhakikisha linakusanya takwimu kutoka balozi zote za Tanzania kujua mahitaji halisi ya walimu na wataalamu wa Kiswahili.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pauline Gekul amesema ili baraza hilo lifanye kazi zake kwa ufanisi ni kuhakikisha linapatiwa fedha za kutosha za miradi ya maendeleo zitakazosaidia pia kubidhaisha lugha ya Kiswahili.

Amesema miongoni mwa mambo muhimu ya kuharakisha ni pamoja na kulisaidia baraza hilo wapatikane mtafsiri wa lugha ya Kichina, mwalimu wa Kiswahili kwa wageni na mwalimu wa ukalimani.

Mkurugenzi wa Utamaduni wa wizara hiyo, Dk Emmanuel Temu amesema wamejipanga kuendeleza ushirikiano na taasisi zote zilizopo chini ya wizara hiyo ili kuhakikisha matumizi ya Kiswahili sanifu yanaendelezwa.

Naye Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolota Mushi amesema baraza hilo hadi sasa tayari limefanya ushawishi na kuwezesha kufunguliwa vituo vipya vya kufundisha Kiswahili katika nchi za Korea Kusini, Italia, Sudan Kusini, Abu Dhab, Comoro, Malawi, Afrika Kusini na kasi hiyo itaendelezwa mwaka huu.

Alisema ipo haja sheria kuangaliwa inayolipa mamlaka baraza hilo kupitia vitabu vya kiada pekee ili kuvipa ithibati, iongezewe wigo hata ipitie vitabu vya ziada kwani vimekuwa vikipenyezwa shuleni na mitaani huku baadhi vikiwa na lugha na maudhui, yasiyoendana na maadili ya Kitanzania.

"Tumezuia kitabu kimoja kuingia mtaani kutokana na maudhui yake na lugha iliyotumika, ipo haja vitabu vya ziada kutungiwa sheria vipite Bakita," amesema Mushi ambaye ni mtaalamu wa Kiswahili.