Rais Samia asamehe wafungwa 2,244

Rais Samia Suluhu Hassan alipohudhuria maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma leo Jumamosi Desemba 9, 2023.

Muktasari:

  • Katika mwendelezo wa sherehe za uhuru wa Tanzania Bara leo Desemba 9, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 2,244.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 2,244 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika.

Kati ya wafungwa hao, 263 wataachiwa huru leo Desemba 9, 2023 huku wafungwa wawili waliokuwa na adhabu ya kifo wakibadilishiwa adhabu hiyo na kuwa kifungo cha maisha jela.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, wafungwa wengine 1,979 wamepunguziwa sehemu ya adhabu zao ambazo wataendelea kuzitumikia gerezani.

“Ni matumaini ya Serikali kwamba wafungwa walioachiwa huru leo Desemba 9, 2023 watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa letu, na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Rais ametoa msahama huo kupitia mamlaka aliyopewa chini ya Ibara 45(1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa msamaha kwa wafungwa kwa kufuata masharti.

Miongoni mwa masharti hayo ni wafungwa wote wenye sifa stahiki wakipunguziwa robo ya adhabu baada ya kutoa punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.

Wafungwa hao ni wale waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka miwili na kuendelea,  ambao wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na ambao waliingia gerezani kabla ya Oktoba 12, 2023.

“Miongoni mwa wafungwa waliogushwa katika msamaha huo ni wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua ya mwisho. Ambapo ugonjwa na hatua hiyo vimethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mkuu wa mkoa au mganga mkuu wa wilaya.

Wengine ni wafungwa wa maisha ambao wametumikia vifungo vyao kwa muda wa miaka 15 na kuendelea.

“Pia kwa wafungwa wote waliobadilishiwa adhabu hesabu zao zitaanza kuhesabika tarehe ya kubadilishiwa adhabu,” imesema taarifa hiyo.

Wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 na zaidi ambao wametumikia robo ya adhabu zao, baada ya umri wao kuthibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au mganga mkuu wa wilaya.

Pia wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani au wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya, Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi, baada ya ulemavu wao kuthibitishwa na jopo la  watalamu wa afya.

Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 10 au zaidi.

Hata hivyo, msahama huo haukuwahusu wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje chini ya Sheria ya Bodi za Paroli Sura ya 400 (R.E 2002), Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291 (R.E, 2002) na Kanuni za kifungo cha ne (The Prisons (Extra Mural Penal Employment) Regulations, 19681.

Pia wale ambao walihukumiwa kifungo kwa mashauri au kesi za uhujumu uchumi na  wanaotumikia vifungo kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, rushwa, usafirishaji kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya ikiwemo bangi.

 “Pia hii haiwahusu wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kujamiiana, utekaji au wizi wa watoto, kupoka, kuwapa mimba wanafunzi au makosa yoyote  yanayohusiana na ukatili dhidi ya watoto na kujihusisha kwa namna yoyote ile a usafirishaji haramu ya binadamu,” imesema taarifa hiyo.

Wengine ni waliokuwa na makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, unyang'anyi wa kutumia nguvu, silaha, kumiliki silaha, risasi, milipuko au kujaribu kutenda makosa hayo, wote hawahusiki na msamaha huo.

“Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali au ujangili, makosa ya wizi au ubadhilifu wa fedha za Serikali si miongoni mwa wanufaika,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.